Hatimaye Vijiji ndani ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa pwani vimebahatika kuendeleza Miradi mbalimbali kupitia mapato ya ndani katika kipindi cha mwezi Julay hadi Septemba ya mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo kwa kipindi hiko kiasi cha Shilingi Bilioni Moja zimeelekezwa katika miradi ya Maendeleo
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa Flex Garden Mkuranga kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi katika Kata, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde alisema pesa hizo za mapato ya ndani zimelenga kutatua changamoto katika sekta ya Elimu, Afya na Mikopo kwa Wajasiriamali.
Munde ambaye pia ni Katibu wa Kikao hicho alitaja utekelezaji huo wa Ilani ya uchaguzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 umelenga katika kumalizia majengo ya Zahanati, Nyumba za Walimu na Madaktari, kujenga Madarasa sambamba na kutoa Mikopo katika vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha Mhandisi Munde alitumia fursa hiyo kuwaomba Madiwani kuhakikisha fedha zinazopelekwa Vijijini miradi yake ilingane na ubora wa ujenzi huku akiwataka watendaji Kata wajipime kupitia usimamizi wa makusanyo katika maeneo yao ili ifanikishe utekelezaji wa Ilani hiyo katika Miradi ya Maendeleo.
Akifunga kikao hiko Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Juma Abeid alimuomba Mkuu wa Wilaya Filberto Sanga kukaa na wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ili kujadili matengenezo ya barabara hususani Vijijini ambako kunakwamisha kupeleka mazao mbalimbali Masokoni na hata kusafirisha Mazao ya Korosho ghalani kwa ajili ya minada.
Juma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Magawa aliwaomba Madiwani wenzake kuhamasisha wananchi ili kujitokeza kwa wiki katika zoezi la kupiga kura Novemba 24 mwaka huu ili kupata Viongozi wa Serikali za Mitaa.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.