Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Waziri Kombo amesema haridhishwi na kiwango cha usimamizi na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa katika kikao kazi kilichofanyika Julai 22, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
Kombo amesema ataendelea kuchukua hatua kali kwa mtumishi atakayesababisha kucheleweshwa kwa mradi au kusababisha mradi huo kutofanyika vizuri, na kwa msisitizo tayari ameanza kuchukua hatua kwa watumishi kadhaa mpaka sasa.
Amesema kwa mwaka huu anataka kila mtumishi akae katika kituo chake cha kazi sambamba na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ili kutoa huduma zilizo bora kabisa.
Sambamba na hayo, amesema hatowavumilia watumishi kuanzia ngazi ya Kata mpaka Kijiji ambao katika maeneo yao Miradi ya Maendeleo haitekelezeki vizuri na kushindwa kumalizika kwa wakati.
Aidha akizungumzia suala la mapato Mkurugenzi amesema ni suala mtambuka hivyo kila mmoja anatakiwa kuwajibika na kuhakikisha Serikali inakusanya mapato vizuri.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Mkuranga Juma Diffa kwa niaba ya watendaji wenzake amemshukuru Mkurugenzi kwa kutoa maelekezo hayo na kuahidi kuwa na utekelezaji mzuri katika majukumu yao.
Kikao hicho kilichowakutanisha Watendaji wa Kata na Vijiji, Waganga Wafawidhi pamoja na Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kilikuwa na lengo la kujadili umuhimu wa kukusanya mapato na kuhakikisha Miradi ya Maendeleo inakamilika kwa wakati kulingana na fedha zinazotolewa.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.