Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa wingi ili waweze kuwa na wigo mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya wilaya hiyo,hayo ameyasema leo wakati wa kikao cha Baraza maalum la Madiwani kujadili taarifa za majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 2019.
“Pamoja na kupata hati safi kwa mara ya nne mfululizo tangu kuanza kwa Serikali ya awamu ya tano niwaombe sana Mkurugenzi Mtendaji na timu yako kusimamia vyema vyanzo vilivyopo lakini pia kuendelea kubuni vyanzo vipya kama ambavyo mmeanzisha mradi mpya wa stendi ya kisasa katika kata ya mwandege mradi ule mkiusimamia vizuri utakua miongoni mwa chanzo kikubwa sana kitakachokuwa kinaingiza fedha nyingi katika Halmashauri hii, alisema”
Aidha katika kuwasilisha hotuba yake Mhandisi Ndikilo alimtaka Kaimu Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Salon Nyika kujipanga na timu yake katika kusimamia mapato na amemtaka ndani ya siku saba kuainisha majina ya wadaiwa wote ambao wengine ni watumishi wa serikali waliopewa dhamana ya kukusanya mapato kwa ajili ya Halmashauri lakini wamekua sio waaminifu na matokeo yake wameshindwa kuwasilisha fedha za makusanyo Benki na hivyo kupelekea hoja za mapato kutokufutika “ Hivyo nawataka ndani ya siku saba warejeshe fedha zote kabla hatua za kinidhamu na kisheria hazijachukuliwa”, alisisitiza.
Aliongeza kwa kusema Mkuranga ni Halmashauri inayokusanya vizuri mapato katika Wilaya zote za Mkoa wa Pwani na mpaka kufikia leo asubuhi ya mwezi Juni na kusema kiwango cha ukasanyaji kwa mwaka huu wa fedha, kimekusanywa kiasi cha shilingi bilioni 5.99 sawa na aslimia 95 wakati lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha ni bilioni 6.31 ambapo kimsingi kimebaki kiasi kidogo sana kuweza kufikia malengo. “Nawaomba msimamie vema makusanyo, na kwa wale ambao wanafanya mzaha katika kutufanya tushindwe kufikia malengo basi Mkurungenzi Mtendaji kwa ushirikiano na wataalamu wa fedha simamia hilo ili kulinda dhamana uliyopewa ya kuongoza Halmashauri hii”
Pamoja na hayo Mhandisi Ndikilo alimtaka mkaguzi wa ndani Bi. Faidha Kassim kusimamia ufutaji wa hoja zote zilizosalia pia awe anatolea taarifa za utekelezaji hoja mara kwa mara.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.