Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani imeingia Mkataba wa upembuzi yakinifu na Kampuni ya ‘Mhandisi consultant Limited’ kwa ajili ya kuandaa andiko la Mradi wa ujenzi wa Stendi kubwa ya Mabasi na Daladala ambao unatarajiwa kuanzishwa na Halmashauri ya Mkuranga hivi karibuni.
Mradi huo wa ujenzi wa stendi unatarajiwa kuanzishwa katika Kijiji cha Kipala Mpakani Wilayani Mkuranga ambapo kumetengwa ekari (50) kwa ajili ya Miradi mbalimbali ya Halmashauri ili kufanikisha lengo la kujiongezea mapato ya ndani.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la kutia saini, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde amesema lengo la kufanya upembuzi yakinifu ni kurahisisha mipango na taratibu ili Mradi huo ukianza ujenzi wake na kukamilika uweze kuimarisha vyanzo vya mapato.
Munde amewasisitiza watendaji wa Kampuni hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuwaahidi wakifanya vizuri na Halmashauri kuridhika na kazi hiyo basi hawatosita kuwapa majukumu mengine katika Miradi mingine ambayo inatarajiwa kufanywa na Halmashauri hiyo.
Nae mwakilishi wa (TIB) Paulo Kanyala amemtaka mkandarasi kufanya kazi ikiwezekana usiku na mchana ili kuendana na kasi ya Mradi huo wa Mkakati ambao utamaliza kabisa changamoto ya upatikananji pesa katika miradi ya maendeleo.
Zoezi hilo linatarajia kugharimu kiasi cha Sh. Million (500) kabla kwa kuanza ujenzi wa Mradi huu Mkubwa utakaohudumia abiria mbalimbali wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini sambamba na kutengwa kwa maeneo ya Wafanyabiashara ndogondogo “Machinga” na fremu za Biashara.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.