Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga imetenga kiasi cha Tshs 431,871,331 ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake na vijana na usimamizi kwa mwaka 2017/2018 na pia kiasi cha Tshs 92,084,500 ni kiasi cha fedha ambacho kitakopeshwa kwa kipindi hiki kwa vikundi vya wanawake na vijana.Hayo yalisemwa leo na Afisa maendeleo ya Jamii Wilaya Bwana Peter Nambunga wakati wa kikao cha kamati ya mikopo Wilaya.
Bwana Nambunga aliendelea kusema kwamba Kwa mwaka huu jumla ya vikundi 60 vya kiuchumi vya wanawake na vijana viliomba mkopo na kati ya hivyo vikundi 29 ni vya wanawake na 31 ni vya vijana vyenye thamani ya jumla ya Tshs 281,478,000/=
Aidha Mratibu wa Mikopo ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii bi Amina Hoja alisema pamoja na maombi hayo kuwa mengi na kiasi cha fedha kilichopo kuwa kidogo Idara ya Maendeleo ya Jamii iliweza kuvitembelea vikundi hivi na kujua hali halisi ya miradi iliyoombewa na kubaini baadhi ya changamoto ikiwemo miradi kutoonyesha uhalisia wa kuombea mkopo na wengine kukosa kabisa shughuli za kufanya hivyo kutokana na hilo Idara baada ya kufanya tathmini ya pamoja na kamati ya mikopo Wilaya imeridhia vikundi 40 kupewa mikopo ambapo vikundi vya wanawake 16 na Vijana 24 ambapo kiasi cha Tshs 92,084,500 kitakopeshwa kwa vikundi hivyo.
Bwana Jafari Mulike Katibu wa kikundi cha KIVIKI Youth Group kilochopo Tengelea alisema”kikundi chetu kinajishughulisha na ufugaji wa kuku wa kienyeji tulikopeshwa kiasi cha Tshs 3,000,000 tangu April 2017 na tunaendelea vizuri na marejesho lakini pia tumepata mafanikio kwani tulianza na kuku 32 lakini sasa hivi tuna kuku 120”
Bi lenada Ndimbo katibu wa kikundi cha wanawake kiitwacho KARIBU FARM kilichopo Mkuranga mjini alisema anashukuru sana kwa Halmashauri kutoa kipaumbele kwa vikundi vya wanawake katika kupata mikopo lakini pia amewasihi wanawake wote wa Mkuranga kujiunga na vikundi mbalimbali vya kiuchumi ili kupata fursa ya kupata mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto ya baadhi ya vikundi kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati,vilevile malalamiko kuhusiana na kiasi kidogo kinachotolewa kulingana na mahitaji halisi.
Mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ilitenga Tshs 221,251,305/= kwenye vyanzo vyake vya mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha vikundi vya kiuchumi vya wanawake na vijana.
Aidha Halmashauri iliweza kutoa kiasi cha Tshs 199,200,000/=kwa ajili ya kukopesha jumla ya vikundi 98 vya wajasiriamali, kati ya hivyo vikundi 46 vya wanawake na 52 vya vijana.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.