Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh Filberto Sanga amezitaka Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Pwani kuwa na sheria ndogo za kudhibiti Sherehe na shughuli mbalimbali zenye kuleta viashiria vya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Sanga aliyasema hayo leo hii kwenye maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambapo alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng Evarist Ndikiloambapo yamefanyika kimkoa katika wilaya ya Mkuranga katika kata ya Mwarusembe.
Sanga aliongeza kwamba anatambua umuhimu wa mila na desturi za wananchi wa Mkoa wa Pwani hasa kwenye uchezaji wa ngoma lakini ngoma hizo zinachezwa bila staha wala nidhamu huku watoto wadogo wakishuhudia na hivyo kuashiria kuleta maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI.
Sanga alibainisha kwamba kipindi hiki cha msimu wa korosho kumeibuka tabia ya wanawake kubadilishana miili yao na korosho ambapo maambukizi mapya ni rahisi kuongezeka kwa msimu huu.
Mratibu wa UKIMWI Wilaya ya Mkuranga Bi Juliana Swai alisema Halmashauri imetoa mafunzo ya stadi za Maisha kwa vijana 350 waliopo nje na ndani ya shule ili kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,Pia wamepewa mafunzo ya ujasiriamali ili wasiwe tegemezi.
Mratibu huyo aliongeza kwamba changamoto kubwa iliyopo ni wanaume wengi kutopenda kupima Virusi vya UKIMWI kwa hiari na vijana kwenye umri mdogo kushiriki ngono isiyo salama na hivyo maambukizi mapya kuongezeka.
Aidha Bi Swai alibainisha kwamba mikakati iliyopo ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wote na kutoa huduma kwa familia zenye wagonjwa wa UKIMWI.
Umoja wa Mataifa uliamua siku ya tarehe 1.12 ya kila mwaka kuwa siku ya Kimataifa ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI kwa lengo kupima na kutathmini kiasi cha utekelezaji wa malengo na maazimio mbalimbali kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2018 yameenda na kauli mbiu isemayo Pima,Jitambue,Ishi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.