Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya na Miji ambao wamepata fedha kutoka serikalini kwa ajili ya kujenga vituo vya Afya wafanye hivyo haraka iwezekanavyo.
Ameyasema hayo jana katika Mkutano maalum wa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega katika viwanja vya Godauni Mkuranga na kuwaeleza ifikapo tarehe 15 mwezi wa kwanza 2020 asiyetekeleza agizo hilo basi aandike barua mwenyewe ya kujieleza kwa nini asiachishwe kazi.
amesema fedha hizo ni za awamu ya pili ya kuendeleza juhudi za Mh. Raisi John Pombe Magufuli kwa kuongeza kujenga vituo vingine vya afya 52 kote nchini ambapo kwa Halmashauri ya Mkuranga imebahatika kupata tena fedha hizo, baada ya fedha za awali ambazo zimefanikisha kujenga vituo vya Afya vya Mkamba na Kisiju na cha tatu ambacho kinatarajiwa kujengwa Vikindu katika Zahanati ya Ngunguti.
Awali Waziri Jaffo alizindua huduma ya X-ray na Utrasound katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga pamoja na Kukagua Miradi mikubwa ikiwemo ya Maji ambao unatarajiwa kukamilika mwezi wa tano 2020 wenye gharama ya shilingi bilioni 5.6 sambamba na jengo jipya la kisasa la wazazi ambalo nalo amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga Mshamu Munde kuhakikisha hadi mwezi wa nne liwe limekamilika.
Nae Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Pwani Zainabu vulu amemuomba Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Afya Ummy Mwalimu kuongeza wataalamu katika Hospitali hiyo kwani imeelemewa na ina uwezo wa kuhudumia wazazi (kuzalisha) akina mama 80 tuu kwa mwezi tofauti na sasa ambapo wanahudumia wazazi zaidi ya 300 kwa mwezi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkuranga Ally Msikamo kwa niaba ya Wazee na Wananchi wa Mkuranga wamemuomba Waziri Jaffo kumfikishia salamu na pongezi nyingi Mh Rais Magufuli na kumuomba afike Mkuranga kuzungumza na wananchi hao kwani wanahamu kubwa sana na yeye, na wanamuunga mkono kwa juhudi zake za kutekeleza ahadi zake kwa watanzania.
Barabara ya Mkuranga Kisiju kuendelea kujengwa kwa kiwango cha Lami baada ya kuongezwa kilometa 5 kutoka ilipoishia sasa hadi kufikia Mbezi na miradi hii inatekelezwa kwa fedha zinazotokana na kodi za wananchi. b
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.