Kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira Halmashauri Wilaya ya Mkuranga imemuagiza Mhandisi wa Ujenzi Shaidu Moudrica kuhakikisha ujenzi wa nyumba anayotakiwa kuishi Mkurugenzi inakamilika mapema iwezekanavyo kabla ya vikao vijavyo ili Mkurugenzi aliyopo sasa aweze kuhamia katika nyumba hiyo.
Kamati hiyo imetoa agizo hilo jana katika kikao cha majumuisho baada ya kufanya ziara ya kukagua baadhi ya vikundi vilivyopata Mkopo kutoka Halmashauri sambamba na miradi ya ujenzi wa ukuta katika nyumba hiyo pamoja na ujenzi wa ukuta kuzunguka jengo la Ofisi ya Mkurugenzi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hassani Dunda amesema kuhamia kwa Mkurugenzi katika nyumba hiyo kutasaidia gharama wanazotumia kwa sasa za kulipa kodi ya nyumba ya Mkurugenzi zitasaidia katika kufanya kazi katika miradi mingine.
Awali wakikagua miradi na vikundi hivyo Kamati imepongeza vikundi vilivopata mikopo kwa kuzisimamia vema fedha hizo na kuzitumia vizuri kwani wameridhika baada ya kuona shughuli zinafanyika vizuri na kuwaasa kuendelea kushirikiana vema na hatimae wahakikishe wanarudisha mikopo hiyo kwa wakati ili waweze kukopa tena.
Ziara ya Kamati hiyo ya kukagua miradi iliyopewa fedha katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2019/2020 imekagua miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 168 ambayo ni vikundi vinne vya vijana pamoja na ujenzi wa ukuta katika nyumba ya Mkurugenzi na ujenzi wa ukuta wa Ofisi ya Mkurugenzi.
Aidha Wataalamu wametakiwa kusimama katika nafasi zao kwa maana ya kufuata taratibu za fani zao sambamba na Afisa Maendeleo Jamii Wilaya ya Mkuranga kuwasilisha majina ya Vikundi vyote kwa Kamati hiyo vinavyodaiwa kwa Kipindi kirefu ili iweze kusaidia na kufanikisha kurudishwa kwa madeni hayo.
Kamati hufanya ziara hizi kwa lengo la kukagua na kuhakikisha fedha zinazotolewa na Halmashauri zinawafikia walengwa na kufanya kazi kama ambavyo wao wamepitisha kupitia vikao vya Madiwani na kuangalia thamani ya fedha hizo na kazi zinazofanyika.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.