Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imetoa mafunzo ya uhamasishaji wa wataalamu ya namna ya kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha mpango wa uhaulishaji katika kata 14 mwanzoni mwa mwezi machi 2018.
Akizunguzumza wakati wa uhamasishaji huo katika kata ya Mkuranga Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) bwana Timoth Kudra alisema kata ambazo zimeshafanya vikao vya uhamasishaji ni kata 14 kati ya 18 ambazo ni Mkuranga,Vikindu,Kiparang’anda,Shungubweni,Mbezi,Kisiju,Magawa,Lukanga,Njianne,Mkamba,Bupu,Kimanzichana,Panzuo na Nyamato.
Mratibu huyo aliongeza kwamba lengo la uhamasishaji huu ni kuwajengea uwezo watendaji wa kata,Maofisa Maendeleo ya Jamii,Maofisa Ustawi wa Jamii,Watendaji wa Vijiji ambavyo mpango upo, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati.
Bi Zubeda Mkupeta Afisa Afya alisema kikao cha uhamasishaji kimemsaidia kujua vema majukumu yake katika mradi huu ambapo anatakiwa kuhakikisha anadhibiti kinga kwa watoto wa umri wa 0-5 na kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo na kuhudhuria kliniki kwa wakati stahiki pia kuhamasisha kaya zote kujiunga na Mfuko wa afya ya jamii(CHF).
Bwana Ame Mnyanga Afisa Mtendaaji wa kata ya Panzuo alisema kikao cha uhamasishaji kimemsaidia kufahamu zaidi kuhusu mradi wa TASAF na malengo yake makuu ya kuweza kuwajengea uwezo kaya maskini na kwenda kwenye hali nzuri ya maisha.
Mnyanga aliendelea kusema watendaji wa kata, vijiji na wataalam wengine wamefanikiwa kutambua kwa urahisi majukumu yao na hivyo kuwapelekea kufanya kazi kwa bidii na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Tasaf awamu ya tatu-Mpango wa kunususru kaya maskini unawezesha kaya maskini kupata mahitaji ya msingi, kulinda rasilimali zao na kuweka akiba kwa ajili ya kujiletea maendeleo na hatimae kujitoa kwenye umaskini.
Madhumuni ya TASAF awamu ya tatu ni kuziwezesha kaya kupata mahitaji ya msingi na fursa za kujiongezea kipato.Walengwa wa mpango ni kaya maskini katika maeneo yaliyoainishwa.Maeneo yaliyotiliwa mkazo ni kunusuru kaya maskini kwa kuzipatia fedha ambazo zitasaidia kwenye uzalishaji mali ili wapate manufaa ya muda mrefu,pia kutoa ajira za muda mfupi kwa walengwa wenye uwezo wa kufanya kazi kutoka kwenye kaya maskini na kuzipatia ustadi mbalimbali, pia kukuza na kuchochea utamaduni wa kaya maskini kujiwekea akiba na kuzipa elimu ya masuala ya fedha na uendeshaji wa biashara ndogondogo, pia kuwezesha jamii maskini kujenga/kuboresha miundo mbinu ya maji, elimu na afya katika maeneo ambayo hayana huduma hizi ili walengwa wapate huduma hizi ikiwa ni kigezo cha kutimiza masharti ya mpango
Wilaya ya mkuranga ina kaya 51,101 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 na TASAF ime wezesha kaya 4690 kwa vijiji 77 kati ya 125.Mpango huu ulizinduliwa septemba 2014 na utekelezaji wake ulianza julai 2013.Mpaka kufika februari 2018 Wilaya ya Mkuranga imetumia jumla ya Tshs 2,828,156,000 katika zoezi la uhaulishaji katika kaya maskini.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.