Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge Amewataka wananchi wa Mkuranga kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Kliniki ya Ardhi ili kuweza kumaliza migogoro ya ardhi Wilayani humo.
Akiongea kwenge uzinduzi wa Kliniki hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki hii katika Kijiji cha Vikindu, Kunenge amesema ni muhimu kwa wananchi wa Mkuranga kushiriki na kuwasilisha kero zao katika Kliniki hiyo kwani ni utekelezaji wa kampeni ya tokomeza migogoro ya Ardhi Mkoa wa Pwani
Amesema Serikali itawachukulia hatua kali matapeli wote ambao watapatikana kwa kuwaongopea na kuwatapeli Wananchi ardhi zao pamoja na wale wanaowachangisha fedha wananchi hao kwa lengo la kuwalipa wataalam wa mambo ya jadi kwa nia ya kufifisha baadhi ya matakwa yao.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir Ali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa amesema wamechagua Kata ya vikindu kufanya Kliniki hiyo kwa sababu ndiyo Kata inaongoza kwa migogoroya ardhi ndani ya Wilaya lakini ndiyo Kata pekee inayoongoza kwa wingi wa watu na shughuli za kiuchumi.
Aidha amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Waziri Kombo pamoja na Mkuu wa Idara ya ardhi Saidi Swalehe kwa kazi kubwa inayofanywa ya upangaji wa miji sambamba na utatuzi wa migogoro unaoendelea.
Amesema mpaka sasa zaidi ya hati 8000 zimeshatolewa kwa wananchi ambao wamefanikiwa kukamilisha taaratibu za umiliki pamoja na kutambuliwa kwa vipande vya viwanja 141,000 ambavyo vimewezeshwa na kuandaliwa kwa michoro ya mipango miji.
Sambamba na hilo ameyataka makampuni ambayo yanaingia vijijini na kupima maeneo kwa ajili ya kuuza viwanja lazima wawasiliane na Idara ya ardhi ili kuweza kupanga mji kwa taratibu zinazohitajika.
Diwani wa Kata hiyo Mohamedi Maundu amewataka wananchi kuitumia fursa ya uwepo wa kliniki hiyo ndani ya kata yao ili kuweza kupunguza au kumaliza migogoro ya ardhi ndani ya kata na Wilaya kwa ujumla.
Katika uzinduzi huo wananchi walipata fursa ya kuwasilisha kero zao na kupatiwa majibu hapo hapo, na Kliniki hiyo itadumu hapo kwa muda wa siku nane tangu kufanyika kwa uzinduzi huo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.