Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani limefanya mabadiliko ya matumizi ya fedha kutoka katika Miradi mingine na kuzipeleka fedha hizo katika sekta ya Elimu kwa lengo la kuongeza Madarasa katika majengo ya Shule za Sekondari hatimaye kuhakikisha agizo liliotolewa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa la kuhakikisha wanafunzi wote waliokosa nafasi katika uteuzi wa awali wawe darasani na wamekaa katika Madawati linakamilika ifikapo Februari 28 mwaka huu,
Akiwasilisha Miradi iliyobadilishwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhandisi Mshamu Munde ameitaja ni pamoja na Mazingira, Mifugo, Ardhi na Miradi mingine ni Maliasili, Fedha na Ujenzi ambazo zote zitagharimu kiasi cha shilingi Milioni 535.5.
Aidha zoezi hilo litaendana na utengenezaji wa Madawati na matundu ya Vyoo sambamba na kuhakikisha wanajipanga vema kukabiliana na changamoto hizo kwa mwaka ujao kwa kujenga madarasa zaidi na ikiwezekana kujenga hata shule mpya shikizi za sekondari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mohamedi Mwela aliwapongeza Madiwani kwa kukubali mapendekezo ya Kamati ya Fedha na Mipango huku akiziagiza kamati za Maendeleo za Kata kuhamasisha Wazazi kuchangia chakula Mashuleni ili kumfanya wanafunzi awe na uelewa mpana na kumwezesha kufanya vizuri akiwa darasani.
Mwela alitumia fursa hiyo kuliomba Baraza hilo kuanza mchakato wa kuanzisha Mamlaka ya Mji mdogo wa Mkuranga hatimaye kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa wananchi wa Mkuranga kwa ujumla.
Akitoa salamu za Serikali Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga aliagiza Walimu Wakuu kutochangisha wanafunzi mara wanapoajiunga na kidato cha kwanza au Darasa la Kwanza huku akimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri Mhandisi Mshamu Munde awataje wafadhili mbalimbali wanaochangia katika Miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuwatia moyo.
Halmashauri inahitaji kuongeza jumla ya vyumba 73 vya Madarasa, vyoo matundu 166 na Madawati 3627 ili kuwezesha wanafunzi 3627 waliokosa nafasi kupata nafasi hiyo mara ifikapo Februari 28 Mwaka huu.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.