Baraza la madiwani wanaounda Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa pwani, wamefanya maamuzi magumu likiwemo kufuatilia kwa karibu mifugo ya Ng’ombe iliyovamia mashamba na kuharibu mazao ya wakulima.
Akijibu maswali ya papo kwa papo katika kikao cha robo ya nne na mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa flex Garden Kiguza Mkuranga, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Juma Abeid alisema wametenga shilingi milioni 17 ili kuendesha operesheni endelevu kubaini ng’ombe waliongia kinyemela ndani ya Wilaya ya Mkuranga.
Akiendelea kufafanua malengo ya opereshi hiyo amesema lengo kuu la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa Wilaya ya Mkuranga inakuwa salama kwa kuwaondoa Ng’ombe wote na kuwarejesha walikotoka ili kuepusha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Juma ambaye pia ni Diwani wa kata ya Magawa alifika mbali zaidi kwa kuweka bayana changamoto sugu ya kuvamiwa maeneo ya ardhi na Wilaya jirani za Kisarawe, Temeke, Kibiti, Ilala na Kigamboni huku wakimuomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi William Lukuvi aje na wataalam wake ili kutatua kwa kuzingatia kwa sasa wilaya zote zinaelekea katika chaguzi za Serikali za Mitaa.
Aidha ameiomba Timu ya uhakiki wakulima wa Korosho Wilayani humo kwenda mashambani ili kujiridhisha uwepo wa Kangomba huku akitoa mfano wapo ambao wa kilo 300 bado hawajalipwa kwa kisingizio hicho cha kangomba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde aliwahakikishia Madiwani suluhisho la migogoro ya Wafugaji na Wakulima itafikia tamati karibuni kufuatia maboresho ya sheria ndogo ya mifugo inayosubiri Baraka ya Wizara ambayo itatoa adhabu ya kutaifisha na kupigwa mnada mifugo inayozagaa.
Munde ambaye ni katibu wa kikao hicho alitangaza uwepo wa kikao cha wadau wa muhogo wiki hii ambacho kitawashirikisha wanunuzi na Mashirika mbali mbali katika sekta ya kilimo cha muhogo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.