Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Filberto Sanga amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kuachana na makundi na kufanya malumbano yasiyo na tija na badala yake kuwa na ushirikianao baina yao kwa faida ya Halmashauri pamoja na wananchi katika Kata zao.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika kufunga Semina ya siku mbili ya Baraza jipya la Madiwani iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Wilaya jana, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mhandisi, Mshamu Munde amesema ofisi ya Mkuu wa Wilaya iko tayari kushirikiana na Madiwani hao na kusisitiza kuwa hatosita kutoa ushauri au maagizo pale atakapoona mambo hayaendi sawa.
Munde amewahakikishia Madiwani hao kuwa hawakuzuiwa kuijadili na kuikosoa taarifa iliyowasilishwa katika kikao cha kwanza cha baraza hilo isipokuwa changamoto zilizoonekana zitajadiliwa na kufafanuliwa vizuri kupitia vikao vya kisheria na kwa mujibu wa kanuni.
Nae Mkufunzi wa semina hiyo Gerard Zephyrin amewataka Madiwani hao kujikita katika kuzisoma na kuzifafanua vizuri Kanuni mbili walizopewa ambazo ni Kanuni za Maadili pamoja na ile kanuni za kudumu za Halmashauri ya Wilaya ili waweze kufanya kazi kwa weledi na itawafanya kuzijua haki zao na hata kuwawezesha kuendesha Baraza lao kwa kufuata kanuni hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mohamed Mwela akitoa neno la shukrani kabla ya kufungwa kwa semina hiyo amewaasa Madiwani wenzake kuzingatia yale yote waliyofundishwa na wakufunzi na kuwataka kwenda kuyafanyia kazi ili kuleta mafanikio chanya kwa Wananchi.
Sambamba na kupatiwa mafunzo hayo Madiwani hao wameomba kupatiwa mafunzo zaidi mara tuu itakapobidi, tena wakishirikishwa na baadhi ya Wataalam ili kuongeza ufanisi kwao na wataalam hao katika kuleta maendeleo ndani ya Wilaya ya Mkuranga.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.