Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, wamemtaka mfanyabiashara wa kuchimba mchanga katika kijiji cha Koragwa Christopher Lema,aondolewe kutokana na kukiuka taratibu za uchimbaji.
Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata ya Mkamba Mh. Hassani Dunda katika kikao cha madiwani, kilichofanyika hivi karibuni.
Alisema katika taarifa ya vikao vilivyopita vya mabaraza waliomba asitishwe kuchimba mchanga lakini kinachoshangaza mpaka sasa anaendelea kuchimba mchanga.
Diwani wa Kata ya Tengelea, Mh. Shabani Manda alisema kuwa Lema hafai kuendelea kuchimba mchanga katika eneo hilo, kutokana na kuingia mpaka eneo la shule.
Alisema pamoja na kupewa zuio la kutochimba mchanga wao wanashagaa nguvu ya kuendelea kuchimba mchanga ameipata wapi.
Alisema wao wanataka akiacha kuchimba mchanga pia azibe na mashimo katika kijiji hicho.
Pia Manda alisema kuwa, Lema alichukuwa watu kutoka vijiji mbalimbali na kudai wote ni wakazi wa Koragwa ambao wanamuunga mkono ili achimbe mchanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Injinia Mshamu Munde alisema kuwa, Lema alifungiwa kuchimba mchanga, lakini alikwenda Baraza la Mazingira (NEMC), ambapo napo walimzuia asichimbe mchanga.Alisema hata hivyo baadaye NEMC walimruhusu kuchimba mchanga kwa mipaka iliyowekwa.
“Kuna barua ambayo nimeipata kutoka kwa wanakijiji zaidi ya 100,ambao walifanya mkutano na kuomba Lema aendelee kuchimba mchanga,’’alisema.
Kwa upande wake Lema alisema kuwa, anapigwa vita na baadhi ya madiwani ambao hawataki yeye achimbe mchanga, lakini makubaliano ya kuchimba mchanga ni kuwajengea shule ambapo amefanya hivyo kwa kuwajengea madarasa ya kisasa manne, ikiwamo na kuchangia maendeleo katika kijiji hicho.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.