Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ikishirikiana na Cassava Adding Value for Africa (CAVA) wametoa mafunzo ya siku mbili yanayohusiana na uokaji bidhaaa zinazotokana na unga wa muhogo.Mafunzo hayo yalifanyika Wilayani Mkuranga kuanzia tarehe 23-24/05/2017 ambapo yalijumuisha washiriki 64,wanawake 48 na wanaume 16 kwenye ukumbi wa upashanaji habari kiguza ikiwahusisha wakulima na wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Mkuranga.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo meneja wa mradi wa CAVA bi Grace Mahende alisema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza kipato kwa wajasiriamali ili kuweza kuwapatia masoko zaidi hususani soko la muhogo mbichi na mkavu.
Grace aliongeza kwamba”wajasiriamali wanatakiwa wasimame kwenye nafasi yao,kwasababu ni muhimu katika kufungua masoko, mahitaji yataongezeka na kipato pia kitaongezeka”alisema
Aidha bi Grace alishauri wakulima watumie unga bora wa muhogo kwani sio kila unga wa muhogo unatoa bidhaa bora,alisema ili kupata bidhaa nzuri za unga wa muhogo watumie chipper machine na sio unga wa makopa.
Dosa Deus Mkazi wa Mwarusembe anajishughulisha na kilimo cha muhogo na ufugaji ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo ya uokaji bidhaa zinazotokana na unga wa muhogo alisema”Nimehamasika sana kuja kwenye mafunzo kwasababu mimi ni mkulima wa zao la muhogo hivyo nimepata mafunzo namna ya kuongeza thamani kwenye zao la muhogo na sasa nimeelewa namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kama kupika tambi hivyo nikitoka hapa nitatengeneza tambi na kuuza hata hivyo utengenezaji wake ni rahisi zaidi”
Bi Sophia Robert Mkazi wa Mkuranga mjini ambaye anajishughulisha na ujasiriamali alisema mafunzo aliyoyapata atayafanyia kazi kwa vitendo kwa kupika maandazi, kripsi na tambi na kuweka kwenye genge lake ili kujiongezea kipato.
Bi Janeth Mbwambo Meneja wa Mkuranga Cassava Cooperative Joint Enterprises (MKUCACOJE) alisema mafunzo haya yalikuja baada ya kuuza unga wa muhogo kwa watu mbalimbali na walipoona malekezo ya namna mbalimbali jinsi unga huo unavyotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali wananchi hao waliomba wafundishwa namna ya kupika bidhaa hizo.
Akifafanua zaidi Janeth alisema baada ya kuona mahitaji hayo aliwasiliana na Meneja wa CAVA na ombi hilo likakubalika na wamegharamia mafunzo hayo kwa kununua mahitaji mbalimbali ikisaidiana na Halmashauri ya Wilaya.
CAVA inashirikiana na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa zao muhogo wakiwemo wakulima, wasindikaji na watumiaji pamoja na watoa taaluma katika nchi tano za Afrika ikiwemo Tanzania,Malawi,Uganda,Nigeria na Ghana. Mradi huu ni wa miaka mitano na sasa hivi ni awamu ya pili tangu ulipoanza mwaka 2014 na unatarajia kumalizika 2019.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.