Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani,imepiga marufuku wakazi wa Wilaya hiyo na wanafunzi kutovuka katika mito,na badala yake watumie njia za barabara ili kuepuka kuzama katika maji ikiwamo kuumizwa na wanyama katika mito hiyo.
Hayo yalisemwa na mkuu wa Wilaya hiyo,Filbeto Sanga,katika kikao cha robo mwaka cha baraza la madiwani kilichofanyika jana Wilayani hapo.
"Kutokana na mvua kunyesha katika kipindi cha mwezi wa nne na mwezi huu,miundombinu imeharibika na watu wamekuwa wakitumia mito kuvuka kwenda Shule na wengine kwenda kutafuta mahitaji,sasa naomba wanafunzi na wananchi,wasitumie mito kuvuka kwani kuna baadhi ya watu walipoteza maisha pia kuna wanyama wakati katika mito hiyo," alisema.
Alisema kuwa wanafunzi watano walipoteza maisha katika mvua na kuna watu wakubwa ambao wamepoteza maisha,lakini wanawafuatilia ili baraza lijalo idadi yake itajulikana na kuambiwa waliopoteza maisha.
Alisema kutokana na mvua kunyesha miundombinu imeharibika na baadhi ya kaya nyumbani zao zimejaa maji na hali hiyo imesababisha wananchi kuyahama makazi yao.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Juma Abeid alisema kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa kupata hati safi kutokana na kusimamia vizuri miradi ya maendeleo ambayo imekamilika kwa wakati.
Akizungumza katika baraza la madiwani alisema kuwa,serikali kila mwaka wanafanya ukaguzi katika halmashauri zote nchini na kama halmashauri itakuwa haikufanya vizuri inapata hati chafu.
Alisema kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wakuu wa idara na madiwani,wameweza kufanya kazi kwa pamoja na kufanikisha fedha za miradi ya maendeleo kutumika kama ilivyokusudiwa,kukaa vikao kwa wakati na kusimamia fedha vizuri za halmashauri.
"Yote hayo tumeyafanya kwa kushirikiana na wakuu wa idara na madiwani na tukafanikiwa kupata hati safi," alisema Juma Abeid.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.