Migogoro ya ardhi inayoendelea katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, inasababishwa na watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji wanaouza ardhi bila ya kufuata sheria.
Kutokana na hali hiyo, Halmashauri kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inatarajia kufanya uchunguzi katika vijiji vyenye migogoro hiyo ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Mshamu Munde, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kutoa tamko kuhusu mgogoro wa shamba namba 271 ambalo linamilikiwa na mwekezaji Soap and Allied Industry, lililopo katika Kata ya Vikindu
“Hapa kuna migogoro mingi ya ardhi ambayo inasababishwa na wananchi, lakini hata wenyeviti wa vijiji na vitongoji, nao ni miongoni mwa watu ambao wanahusika kuuza ardhi bila ya kufuata sheria,’’alisema.
Alisema Wilaya kwa kushirikiana na TAKUKURU wanafuatalia migogoro hiyo na ikibainika watendaji kuuza mashamba bila kufuata utaratibu hatua za kisheia zinachukuliwa.
Akizungumzia kuhusu mwekezaji Soap and Allied Industry, alisema kuwa mwekezaji huyo anamiliki kihalali ekari 1750, ambazo alipewa mwaka 1988 na kijiji cha Vikindu.
Alisema mwanzoni wanakijiji walilalamikia umiliki wa mwekezaji huyo sio halali, lakini kamati ziliundwa na kufuatilia umiliki huo na kubaini kuwa mwekezaji anamiliki ekari hizo kihalali na sio kweli kuwa ni eneo la wanakijiji.
Hata hivyo, Munde aliwataka wananchi kuepukana na matatpeli ambao wanatangaza hilo eneo linauzwa,pia amewataka wananchi ambao wanahitaji kuwekeza katika Wilaya hiyo au kununua maeneo kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi, wafike katika ofisi za Halmashauri ili kupata mwongozo ambao utawasasaidia kupata maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa makazi ya nyumba.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.