Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Pwani Mh. Hawa Mchafu amewataka wanajamii wote kudumisha amani na kujiepusha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na uhalifu, ubakaji, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe haramu maarufu kama virobo na gongo,ukatili na ukandamizaji wa makundi mbalimbali katika jamii kama vile watoto, wanawake, wazee na wenye ulemavu.
Mchafu alisema hayo wakati wa siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hapo jana yaliyofanyika katika kata ya Nyamato wilayani Mkuranga.
Mchafu aliongeza kwamba pamoja na unyanyasaji juhudi mbalimbali za wadau na serikali katika nchi yetu bado ukatili na unyanyasaji kwa wanawake ni mkubwa mno.”Katika wilaya yetu ya Mkuranga bado vitendo hivi vinaendelea katika baadhi ya maeneo ya kata na vijiji vyetu”. Mchafu alisema
Mchafu aliendelea kusema kwamba tayari serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuondoa tofauti za kijinsia kwa kuingiza mitazamo ya kijinsia katika sera zinazowabagua wanawake “Nitumie fursa hii kuwaasa wanawake kujitokeza kushiriki katika fursa na nafasi mbalimbali na kufanya kazi kwa juhudi,maarifa na weledi mkubwa ili kufikia malengo ya Tanzania ya Viwanda.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga bwana Peter Nambunga alisema Halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia Mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ambapo kwa miaka mitatu jumla ya fedha 366,284,500 kwa vikundi 207, vikundi vya vijana 115 na wanawake 92,vyenye jumla ya wanufaika 3075 ambapo kati yao wanawake 1,959 na wanaume 1,116.
2018/2019 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi cha Tshs 373, 725.040 kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo na inatarajiwa jumla ya wanufaika wanaokadiriwa 756 wanaume na 278 wanawake watanufaika na mikopo hiyo.
Bwana Nambunga aliendelea kusema Halmashauri imefanikisha uundwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ngazi ya kata na vijiji, Aidha majukwaa hayo yameundwa katika kata zote 25 na vijiji 122 na lengo la uundaji wa majukwaa hayo ni kuondoa matabaka na ubaguzi wa kiuchumi kwa wanawake ili kuleta maendeleo ya usawa.
Siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 machi ya kila mwaka ambapo maadhimisho haya husisitiza na kujenga mshikamano kwa wanawake wote duniani, kuhamasisha jamii kutafakari kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake.Maadhimisho haya hutoa fursa kwa wanajamii, serikali,wananchi, wadau na wanawake wenyewe kupima utekelezaji wa maazimio, matamanio na mikataba ya kimataifa na kitaifa kuhusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa kijinsia.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2018 yalienda na kauli mbiu isemayo “kuelekea uchumi wa viwanda,tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake vijijini”.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.