Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba amewaagiza timu ya uhakiki malipo ya zao la korosho nchini kutayarisha na kubandika majina yote ya wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa na kulipwa fedha zao.
Naibu waziri Mgumba ameyasema hayo akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha godown Kijiji cha Mkuranga wilayani Mkuranga mwishoni mwa wiki, akiangalia changamoto mbali mbali hasa zinazohusiana na zao la korosho.
Amesema kubandikwa kwa majina hayo kutapunguza na kuondoa sintofahamu inayoendelea ya kuonekana wakulima wengi hawajalipwa ilihali hadi sasa serikali imebaki na deni la shilingi bilioni themanini tuu kukamilisha malipo hayo kwa wakulima wa korosho.
Aidha Mgumba amewasihi wakulima wa zao hilo nchini kuwa na subira kwani tayari Serikali imepokea malipo ya shilingi bilioni thelathini ambazo muda wowote kuanzia sasa wakulima watafanyiwa malipo hayo.
Pia Naibu Waziri amesisitiza kwa wakulima wa zao hilo kuwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amesema hakuna kangomba ambaye hatolipwa fedha kwa msimu huu kutokana na korosho alizokusanya ghalani na badala yake wanatakiwa kuandika barua ya kukiri kufanya kosa na kuahidi kutorudia tena jambo hilo.
Pamoja na hayo amewataka wamiliki wa viwanda vinavyobangua korosho nchini kujiandaa kwani Serikali imeazimia kuwa viwanda hivyo vitakuwa vya kwanza kupatiwa korosho kabla ili vijana waliopo nchini wapate ajira.
Serikali imejipanga kuandaa utaratibu mpya wa ununuzi wa korosho kwa msimu wa mwaka 2019/2020 ili kuhakikisha Mkulima anapata stahiki yake.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.