Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde amewataka watendaji katika ngazi za kata kutatua migogoro mbalimbali ili kuepusha wananchi wengi kufika Ofisi ya Mkurugenzi kwa lengo la kusaidiwa kutatuliwa migogoro hiyo.
Munde aliyasema hayo hapo jana wakati wa kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Parapanda ambapo kikao hicho kiliwajumuisha watendaji wote katika ngazi za kata wakiwemo Maofisa Kilimo, Maofisa Mifugo na Uvuvi,Maofisa Ustawi wa Jamii,Maofisa Maendeleo ya Jamii na Waratibu Elimu kata.
Munde aliongeza kwamba migogoro mingi huanzia kwenye ngazi zavijiji na kata hivyo ni rahisi watendaji kwenye ngazi husika kujihusisha kutatua migogoro hiyo kuliko kuacha wananchi hao kufika kwenye ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kusaidiwa kutatuliwa migogoro yao wakati kwenye ngazi ya kijiji wanafahamu migogoro hiyo kwa undani zaidi.
Munde alisisitiza kwamba Serikali huanzia kwenye ngazi za vijiji hivyo watendaji kwenye ngazi hizo wahakikishe wanawaaminisha wananchi wao kuhusu utendaji wao ili migogoro inayoletwa kwenye ofisi yake ipungue.
Afisa maendeleo ya Jamii Wilaya Bwana Peter Nambunga ambaye pia alikuwa mratibu wa kikao kazi hicho alisema lengo kubwa la kuwaita watendaji kwenye ngazi za kata ni kuongeza usimamizi, uwajibikaji, ufuatiliaji na upatikanaji wa taarifa kwa ngazi za chini ili kupunguza majukumu na ufatiliaji kwa Mkurugenzi Mtendaji na Mkuu wa Wilaya kwani itajenga ufahamu wa kufanya kazi pamoja kisekta.
Nambunga aliongeza kwamba wanatarajia kikao kazi hiki kitasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za wananchi kupitia mamlaka zao kwa kutoa maelekezo kwa wananchi jinsi gani wanaweza kutatua matatizo katika mamlaka zao za vijiji na kata kabla ya kufika kwa Mkurugenzi Mtendaji au Mkuu wa Wilaya sambamba na kufahamu changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi na namna ya kuzitatua changamoto hizo.
Afisa Mtendaji kata ya Kisiju bwana Juma Katundu alishukuru sana kwa kufanyika kwa kikao kazi hicho na kusema kwamba kimewasaidia kutambua umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano katika ngazi za kata lakini pia watendaji wote katika ngazi za kata watakua wanaongea lugha moja katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Wataalamu hao wamejiwekea mikakati mbalimbali katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na pia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kufikia lengo la utoaji huduma bora kwa wananchi kwa kufanya vikao kazi hivyo kila baada ya miezi minne.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.