Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imehakikishiwa kujengwa kwa Kituo kikuu cha Mabasi yaendayo kusini na Nchi jirani kusini mwa Tanzania katika Kijiji cha Kipala Mpakani kata ya Mwandege na wananchi wa Mkuranga wamekubaliana kukiita kituo hiko kwa jina la “kituo cha mabasi cha Samia Suluhu Hassan”.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa juma lililopita katika mkutano wa wananchi waliokuwa katika kijiji cha Tambani na waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu katika ziara ya kukagua miradi ya Afya, Elimu na Miundo mbinu wilayani Mkuranga,ambapo katika suala la elimu bure kwa shule za msingi na sekondari litaendelea kuwepo na kuwataka wananchi kupuuza taarifa za watu zinazoendelea za kusema Elimu bure inaenda kufa.
Waziri Ummy ameongeza kuwa sambamba na hilo ataongea na viongozi wa DART ili kuona ni namna gani wataweza kufanikisha barabara ya mwendo kasi inafika vikindu kwa lengo la kuifanya Mkuranga kupata huduma bora kulingana na wananchi wengi wanaohamia kwa wingi ndani ya wilaya hiyo.
Aidha Ummy Mwalimu amewahakikishia wananchi wa Mkuranga kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kujenga shule moja ya Sekondari kila Kata sambamba na kumtaka Mkandarasi anayejenga daraja la Mipeko linalogharimu kiasi cha shilingi milioni 200 kumaliza kazi hiyo katika muda uliopangwa.
Nae mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari kunenge amemuhakikishia wao kama Mkoa watajipanga na watashirikiana vema na viongozi wa wilaya ili kuhakikisha fedha zote za Miradi zinasimamiwa vema na watafanya kazi kwa lengo la kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani.
Awali akiwasilisha maombi ya Wilaya hiyo Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega allimuomba Waziri kuwasaidia wananchi wa Mkuranga mambo matatu, ujenzi wa Kituo cha Mabasi yanayokwenda kusini mwa Tanzania, miundo mbinu ya Barabara na Madaraja pamoja na kuiboresha hospitali ya Wilaya ambapo Tayari waziri amesema iko haja ya kujenga hospitali mpya ya wilaya na ile iliyopo itumike kama kituo cha afya.
Akitoa nenO la shukrani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mwamtumu Mgonja amemuahidi waziri kwa niaba ya Rais wao kama Halmashauri watashirikiana kwa kiasi kikubwa katika kukusanya na kuongeza mapato ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Mkuranga.
Madiwani wametakiwa kumuunga Mkono Rais katika jitihada zake za kuleta maendeleo nchini sambamba na kuacha kulumbana na kutakiwa kushirikiana katika kusimamia miradi ya maendeleo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.