Mke wa Rais mama Janet Magufuli amepongezwa na wananchi wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani kufuatia huruma yake kwa watoto wenye ulemavu baada ya kutoa msaada wa baiskeli maalum kumi ambazo zitawasaidia baadhi ya watoto hao wenye ulemavu.
Akizungumza na wananchi katika kilele cha kusheherekea Sikukuu ya Wanawake Duniani iliyofanyika Kiwilaya kwenye Kijiji cha Kisemvule jana, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi Abdallah Ulega amesema msaada huo aliokabidhiwa Ikulu ndogo Jijini Dar Es Salaam wiki iliyopita ni kielelezo tosha ni jinsi gani Rais Dr. John Pombe Magufuli na mkewe walivyo na mapenzi ya dhati kwa wananchi wa Mkuranga.
Katika sherehe hizo Ulega alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde awasimamie watendaji na wataalam wa Kata zote (25) waandae Miradi ya Kimkakati katika sekta mbalimbali hatimaye shilingi Milioni (500.6) zilizotengwa na Halmashauri kwa ajili ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Walemavu zinaleta tija kwa wananchi.
Aidha Mbunge huyo alilipongeza Jukwaa la Wanawake Wilaya ya Mkuranga kwa uwezeshaji kiuchumi kwa kuwa na mikakati ya kuwakwamua wanawake kwa kuviwezesha vikundi Vijijini huku akiwaahidi kuandaa Semina ya kuwajengea uwezo, kuwapa Mifugo ya Kuku na kuwapa Vyerahani (25) katika Kata zote.
Akizungumzia Miradi ya Maendeleo, Ulega alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Magufuli kwa kuipa Halmashauri hiyo mamilioni ya pesa katika Miradi ya Barabara, Umeme, Maji, Elimu na Afya huku akiwaomba wananchi kuonyesha shukrani katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuchagua Rais, Mbunga na Madiwani kupia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Awali Mwenyekiti wa jukwaa hilo Mariamu Ulega, aliiomba Serikali kuangalia kwa karibu kundi la Wanawake kwa kuwaongezea Mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi huku akiwahakikishia wanawake wenzake kuandaa harambee itakayowashirikisha wadau mbalimbali hatimaye Jukwaa hilo liweze kuendesha miradi ya wanawake kikamilifu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wilaya na Kata, ilifungwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisemvule Omari Makunge kwa kuwaomba wananchi kutunza Miradi iliyopo katika Vijiji vyao ili iwe endelevu sambamba na kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.