Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani imeomba serikali kuongeza idadai ya walimu wa masomo ya sayansi ili kuboresha elimu katika wilaya hiyo na kunusuru shule za Wilaya hizo dhidi ya matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Akisoma risala mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh.Prof.Joyce Ndalichako,Afisa Elimu Sekondari Wilaya Bwana Benjamin Majoya alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi kujiunga na elimu ya Sekondari jambo ambalo limesababisha uhitaji wa walimu mkubwa.
Alisema kwa sasa wilaya ya Mkuranga ina uhaba wa walimu 485 ikilinganishwa na idadi ya 1642 ambapo wanahitajika ili kutosheleza mahitaji.
“kwa kiasi kikubwa uhitaji wa walimu ni kwa upande wa masomo ya sayansi ambapo tunahitaji walimu 77” alisema bwana Majoya.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mh.Juma Abeid ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya mawasiliano na Halmashauri ili kujua uhitaji wa walimu katika shule wilayani humo badala ya kugawa walimu katika maeneo yalio na idadi kubwa ya walimu huku kukiwa na maeneo yenye idadi ndogo ya walimu.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof.Joyce Ndalichako Mh Abeid alisema licha ya kuwepo kwa uhitaji wa walimu bado idadi ya walimu wanaoletwa katika wiaya hiyo huwa wanaelekezwa kwenye vituo vyenye utoshelevu.
“Tatizo hili ni kikwazo tena si katika elimu tu pia afya ambako kuna zahanati zina muhudumu mmoja mmoja wakati kuna maeneo mengine yana uhitaji mkubwa”Alisema
Mbunge wa Mkuranga Mh Abdallah Ulega akizungumza mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Joyce Ndalichako alisema Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa maeneo nchini ambayo yana mwamko mdogo wa elimu huku kukiwa na idadi kubwa ya wahitimu ambao hawakufanya vizuri kwenye mitihani yao ya Kumaliza elimu ya sekondari na hivyo kutoendelea na masomo.
Mbunge huyo amemuomba Waziri Ndalichako kutimiza adhma ya muda mrefu ya wananchi wa Mkuranga kwa kusaidia ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) ili kuzalisha wataalamu wengi katika kueleka nchi ya viwanda.
“kwa kipindi kirefu Baraza la Madiwani liliazimia na tukaandaa eneo kwa ajili ya ujenzi,hatutapenda kuona vijana wetu wanaenda kuwa manamba katika viwanda ambavyo vinaendelea kujengwa na kuboreshwa kila kukicha “Alisema
Aidha Waziri Ndalichako amewataka uongozi wa Wilaya hiyo inafanya jitihada na kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinapanda katika wilaya hiyo ili kuunga mkono jitihada za Serikali ambayo inatoa fedha za elimu kila mwezi.
“Jitihada hizi zianze mwaka huu ili tupate matokeo mazuri ya mitihani inayofanyika mwaka huu kwani muda upo wa kufanya mabadiliko na kuleta matokeo chanya” alisema.
Alisema ni jambo la muhimu kwa wananchi kutambua jitihada za serikali inayotoa bilioni 17.7 kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha elimu bure.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.