Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ameahidi kutatua changamoto ya maji eneo la Mkuranga mjini Mkoani Pwani.
Waziri huyo aliyasema hayo hapo jana wakati alipofanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Uongozi wa Chama cha Mapinduzi na Wakuu wa idara mbalimbali baada ya kuona changamoto ya upatikanaji wa maji mjini Mkuranga.
Akisoma Taarifa ya huduma ya maji Wilaya Mhandisi Renard Baseki alisema huduma ya maji wilayani hapa maeneo ya vijijini yamekuwa yakipata maji kwa wastani wa asilimia 62.5 na huduma hii hutolewa kwa kutumia miundombinu ya maji ya mitandao ya bomba, visima virefu na vifupi vya pampu za mkono na zinazoendeshwa na mitambo ya jenereta za nishati ya mafuta, umeme wa mguvu ya jua na mifumo ya kuvuna maji ya mvua.
Aidha Baseki aliendelea kufafanua kwamba jumla ya wakazi 2512 wa makao makuu ya Halmashauri ya Mkuranga wamekuwa wakipata maji safi na salama sawa na asilimia 10 ya wakazi wote wa mji.kijiji hiki hupata maji kutoka katika chanzo ambacho ni kisima kirefu kilichopo eneo la kulungu.
Mhandisi Mshamu Munde Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga alisema” Tuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji hapa mjini Mkuranga, malalamiko kwa wananchi ni mengi sana hivyo tukipata fungu la kutengeneza miundombinu ya maji tutakuwa tumetimiza kiu ya wananchi wetu”
Kufuatia changamoto hiyo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mh Mhandisi Isack Kamwelwe alisema “Mniandikie andiko kwa ajili ya kutatua changamoto hii na andikeni hilo andiko bila kujali bajeti yenu ili nilifanyie kazi”.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh Filberto Sanga aliongeza kwa kusema Wilaya ya Mkuranga ina maji mengi ardhini ambayo ni safi na salama hata viwanda vyote vya Mkuranga hutumia maji hayo kwa matumizi ya viwanda na alimuhakikishia Waziri wa Maji na Umwagiliaji kuandika andiko hilo ili kutatua changamoto ya maji mjini Mkuranga na kupeleka ofisi ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Wilaya ya Mkuranga ina vyanzo vikuu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uvunaji wa maji ya mvua, maji ya chini ya ardhi(Underground Water), Chemichemi na mabwawa. Mpaka juni 2017 jumla ya wakazi 123,623 wanapata huduma ya maji safi na salama, hii ni sawa na asilimia 62.5 ya wakazi wote 197,797 wa Mkuranga waishio vijijini. Vilevile asilimia 10 ya wakazi wa mji wa Mkuranga ndio wanaopata huduma ya maji safi na salama.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.