Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Mhandisi Mshamu Munde ametoa rai kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kujitokeza na kuendeleza juhudi za Serikali katika kutatua na kuziondoa changamoto mbalimbali katika sekta ya Elimu Wilayani humo.
Munde ameyasema leo katika hafla ya kukabidhi baiskeli 30 kwa baadhi ya Shule za Sekondali ili ziweze kuwasaidia wanafunzi wa kike ambao wanatembea umbali zaidi ya kilometa 10 kutoka majumbani mwao kufuata shule ilipo na kuwaondolea vikwazo mbalimbali wakiwa njiani.
Baiskeli hizo ambazo zimetolewa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Forum for Balanced and sustainable development kwa ufadhili wa HASENE Internatinal kwa lengo la kuwasaidia watoto wa kike wa kidato cha kwanza hadi cha tatu.
Awali akiwasilisha taarifa fupi ya changamoto zinazoikumba Halmashauri ya Mkuranga katika sekta ya Elimu, Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Mkuranga Benjamin Majoya ameishukuru taasisi hiyo kwa kuliona tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi kwa kuleta baiskeli na kuwaomba kuendelea kusaidia kwa mambo mengine katika sekta hiyo.
Nae katibu wa taasisi hiyo Chake Bakari ameahidi kupitia taasisi hiyo au hata kupitia taasisi nyingine kuona ni namna gani wanaweza kuendelea kutafuta misaada mingine na hasa zikiwemo ya upatikanaji wa vitabu mbalimbali vya masomo, kompyuta sambamba na miundo mbinu ya Elimu.
Ameongeza kuwa Baiskeli hizo siyo mali ya mwanafunzi bali itakuwa ni mali ya shule husika isipokuwa watakabidhiwa kuzitumia wakiwa shule na wanapomaliza au kuacha shule wanatakiwa kuzikabidhi shuleni ili ziweze kuwasaidia wengine.
Shule zilizobahatika kupata mgao huo kwa baadhi ya wanafunzi wake ni Shule ya Sekondari shungubweni baiskeli 7, Kisiju 10, Mwandege 3, Dundani 5 na Shule ya Sekondari Tengelea baiskeli 5
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.