Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Filberto Sanga ameipongeza kampuni ya Tanzania huafeng Agriculture Development Limited kutoka China kwa kuwekeza kiwanda cha kuchakata muhogo mbichi ndani ya Wilaya hiyo hali itakayochangia wakulima kujikwamua kiuchumi.
Akifungua kikao cha wadau wa muhogo kwenye ukumbi wa kituo cha upashanaji Habari Kiguza, Sanga aliwataka Maafisa ugani Kata zote 25 washirikiane na Kituo cha utafiti wa mazao ( TARI ) Kibaha ili wakulima kwenye Vitongoji wapate mbegu bora na dawa ya kuuwa wanaoshambulia zao hilo hatimaye lilete tija na kuwa mbadala wa zao kuu la korosho.
Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya alimwagiza Mkuu wa idara ya Kilimo umwagiliaji na ushirika ( DAICO ) Julitta Bulali kusimamia uanzishwaji wa mashamba darasa katika kata zote sambamba na kuimarisha vyama vya msingi ( AMCOS ) na vikundi ili vifaidike na mikopo ya Halmashauri ya Wilaya na Taasisi mbali mbali za fedha.
Wadau mbali mbali wa zao hilo walipata fursa ya kupendekeza bei kwa wawakilishi wa kampuni hiyo wakiomba bei waliyopanga Shilingi 80 kwa kilo kuonekana ndogo ukilinganisha na gharama za utayarishai wa mashamba hadi kuvunwa kwa zao hilo.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na Maafisa Tarafa, TCCIA, MEDA na TARI kitaendelea tena Jumatano tarehe 2 octoba baada ya watafiti, wataalamu na Mwekezaji kukutana na kufikia muafaka wa bei halisi itakayokidhi mahitaji ya kila upande kati ya mkulima wa zao hilo pamoja na mwekezaji.
Akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda hicho kilichopo Kijiji cha Mkenge Agosti mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo aliagiza kufanyika kikao hicho sambamba na wilaya zote Mkoani Pwani kujipanga katika kilimo cha muhogo ili kutosheleza mahitaji ya kiwanda hicho ambapo kwa siku kina uwezo wa kupokea tani 200 hadi 1000 za muhogo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.