MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezitaka Halmashauri zote za Mkoa huo kuwa hazitakiwi tena kushangilia wa kupigiana makofi kwa kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na badala yake wajikite kwenye matumizi yenye tija.
Kunenge ameyasema hayo leo tarehe 20 juni 2024 alipokuwa katika kikao cha Baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Mkuranga kujadili hoja za Mkaguzi wa hesabu za Serikali lililofanyika kwenye ukumbi wa Flex Garden kiguza.
Akizungumza katika Baraza hilo Kunenge amesema Halmashauri za Mkoa huo zimekuwa zikipata hati safi kila mara jambo ambalo kwa sasa limekuwa la kawaida na wanatakiwa kubadilika kwa kujikita kwenye matumizi yenye tija kwa kuangalia vipaumbele vya wananchi.
Amesema wananchi wanataka kuona hali halisi kwenye maisha yao ya kila sikuna sio kwenye makaratasi kwa kuandika katika utaratibu wa asilimia.
Aidha amesema kuanzia Mwaka wa fedha ujao kila Mkuu wa idara na Kitengo atawajibika na hoja zake mwenyewe na kwa utaratibu huo utasaidia kutokuwa na hoja katika vipindi vijavyo.
Kadhalika Mkuu huyo wa Mkoa ameelekeza Halmashauri hiyo kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuongeza umahiri wa kukusanya sambamba na kuwa makini kwenye matumizi kwa kutumia maeneo yenye tija.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir alitoa Rai kwa watumishi kuwa waadilifu na kila Mkuu wa idara na Kitengo anatakiwa kukaa na wataalamu wake na kujadili mikakati ya kuinua mapato ya Halmashauri sambamba na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kukaa na timu yake kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaenda kujibu hoja za wananchi ambao ndio walengwa.
Awali akiwasilisha taarifa fupi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Waziri Kombo alisema hoja zote zilikuwa 49 na hadi sasa zimefungwa hoja 31 na hoja 18 zilizobaki zinaendelea kufanyiwa kazi
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.