Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde ameipongeza Kamati ya Afya ya Msingi ndani ya Wilaya hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha watoto kuanzia miezi tisa hadi chini ya miaka mitano wanapata chano ya Surua rubella na Polio, zoezi ambalo lilifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 17 hadi 21/10/2019.
Ametoa pongezi hizo jana katika kikao cha kamati hiyo cha kufanya tathmini ya zoezi zima la chanjo hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya Mkuranga baada ya kuvuka malengo kwa kuwapatia chanjo ya rubella walengwa 35,657 sawa na asilimia 105 wakati walengwa halisi walikuwa 33,920 sambamba na kuwapatia chanjo ya polio kwa njia ya sindano walengwa 19,197 sawa na asilimia 102 wakati walengwa halisi walikuwa 18,745.
Nae mratibu wa chanjo Wilaya ya Mkuranga Anna Liachema akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa zoezi la chanjo hiyo amesema wamefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ingawa kulikuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutokuwepo kwa chanjo za Kampeni za kutosha katika stoo ya chanjo ya Mkoa na kupelekea kutumia chanjo za routine.
Liachema ameongeza kuwa changamoto nyingine ni kuchelewa kwa pesa za kampeni na upungufu wa pesa hizo kulingana na vituo vinavyotoa chanjo na timu za wachanjaji sambamba na kufanya zoezi la kampeni katika kipindi cha mvua.
Zoezi hilo la chanjo lilifanyika katika vituo mbalimbali 42 ndani ya wilaya ya Mkuranga pamoja na vituo vya kuhamahama (mobile) ambavyo vilipangwa sambamba na vituo husika na Kamati hiyo ya Afya ya Msingi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa Halmashauri 9 za Mkoa wa Pwani ambayo inashiriki kikamilifu katika Kampeni mbalimbali za chanjo zinazoendeshwa nchini.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.