Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo amesisitiza kuwa uuzwaji na ununuzi wa zao korosho ndani ya Mkoa huo kwa msimu wa mwaka 2019/2010 utafuata sheria na kanuni za mfumo wa stakabadhi ghalani.
Hayo ameyasema jana katika Mkutano mkubwa uliofanyika katika viwanja vya Godown Mkuranga Pwani na kusisitiza serikali haiwezi kuvunja sheria kwa kuuza Korosho kwa kutumia mifumo mingine zaidi ya mfumo uliopo wa stakabadhi ghalani.
Ndikilo ameendelea kupigilia msumali kwa watu wanaotaka kuharibu mfumo huo na kuwaambia hata kama Korosho hizo hazijapokelewa katika ghala kuu kwa kukosa viwango vilivyowekwa vya daraja la kwanza na pili erikali itasimamia Korosho hizo katika maghala ya vyama vya msingi na zitauzwa kwa mfumo uliwekwa wa stakabadhi ghalani.
Nae Naibu waziri wa Kilimo na Ushirika Omari Mgumba amewahakikishia wakulima zao la Korosho ambazo mwaka huu zimeonekana kukosa ubora unaotakiwa, kuwa korosho zao zitauzwa na kila mkulima atapata stahiki yake pamoja na kuwapongeza kwa msimamo wao wa pamoja wa kutetea maslahi yao katika zao hilo.
Mgumba akijibu hoja ya deni linalodaiwa Serikali kwa wakulima wa Korosho kwa Msimu uliopita, iliyowasilishwa na Mbunge wa jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Abdallah Ulega, amesema Serikali kwa sasa imeshalipa fedha zote kwa korosho ambazo zilikusanywa kupitia maghala makuu na kuwahakikishia wakulima hao kuwa Takukuru inaendelea na uchunguzi kwa wale wote walionekana kukiuka taratibu na kusababisha baadhi ya wakulima kukosa fedha zao hadi sasa.
Ili kuhakikisha Korosho hizo zinauzwa mwaka huu serikali imedhamiria kukutana na wanunuzi wa zao hilo ili kuona ni namna gani wanaweza kununua na kupata vibali vya kusafirisha bila kuathiri sheria na kanuni zilizowekwa.
Wanunuzi wa Korosho wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika mnada unaotarajiwa kufanyika siku ya tarehe 27 mwezi huu kama ambavyo Mkuu wa Mkoa amependekeza.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.