Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Mhe. Hadija Nasri amewataka Wakuu wa Shule za bweni zilizopo ndani ya wilaya ya mkuranga kuchukua tahadhari ya namna ya kukabiliana na majanga ya moto yanayoweza kutokea mashuleni.
Akizungumza katika kikao alichoitisha leo tarehe 26 Julai, 2021 kilichojumuisha Wakuu wa Shule za bweni na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Mkuu huyo aliwawasisitiza wakuu wa shule kuwa na dhana za kuzimia moto katika viunga vyote vinavyoizunguka shule ikiwemo mabwenini na katika mabwalo ya chakula.
Akitoa ufafanuzi wa namna ya kukabiliana na majanga yanayosababishwa na moto Afisa wa jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkuranga A/Insp. Fransisco Chunji amewaomba walimu kuwashirikisha katika ujenzi wa mabweni na majengo ya shule ili kuweza kuwashauri katika kuweka mifumo ya kung’amua moshi kabla madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na moto kutokea.
Aidha, Chunji aliwaeleza walimu hao kushirikiana na Kamati za Shule kujenga utaratibu wa kuzungumza na wanafunzi mara kwa mara kwa lengo la kupata taarifa za Watoto ambao wanaweza kuwa chanzo cha majanga hayo kutokana na utovu wa nidhamu au kutokuridhishwa na huduma zinazotolewa mashuleni na hivyo kufanya hujuma kati ya wanafunzi, wanafunzi na walimu au wananchi kutoka nje ya shule.
Askari huyo aliwataka walimu kuchukua tahadhari ikiwemo ukaguzi wa majengo ambayo yamekaa mda mrefu yanayoonesha hali ya uchakavu kufanyiwa ukarabati wa kuta nenye nyufa na mifumo ya umeme.
Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Mshamu Munde aliyewakilishwa na Afisa Elimu Wilaya Mwalimu Benjamini Majoya, amewataka walimu kufanya mabaraza angalau mara moja kwa muhula ili kuwaruhusu wanafunzi kusema nini wanataka katika madarasa yao na mabweni ili kupata picha ya changamoto na shida zinazowagusa na kupitia hayo unaweza kupata taarifa za mambo yanayowasibu, mfano kuna mwalimu anachapa sana, kutokujua hilo kunaweza kusababisha wanafunzi kuchukia na kutafuta upenyo wa kuwasilisha hisia zao kwa kufanya uharibifu wa miundo mbinu kwa kutumia njia za Kuchoma moto au kuvunja vifaa vya kusomea
“Watoto kama jamii na familia ya shule mbinu mbali mbali zinaweza kutumika lakini ni muhimu kuwapa majukwaa ya kusemea changamoto zao” alisema.
Akihitimisha Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Ally Mbikilwa alitoa ufafanuzi juu ya tahadhali ya ugonjwa wa UVIKO19 na kuwataka walimu kuchukua hatua kama miongozo na maelekezo ya afya yanavyotolewa na Serikali ili kuikinga jamii ya shule kwa ujumla.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.