Mkuu wa wilaya Mkuranga wa Mkoa Pwani Mhe. Hadija Nassir ALi ametoa maagizo kwa Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Kata na vijiji kuwa mabalozi katika utunzaji wa mazingira yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya ufugaji wa nyuki sambamba na upandaji wa miche ya Miembe.
Hayo ameyasema leo Mei 20, 2022 katika shule ya msingi Lukanga wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya nyuki Duniani.
Mh. Hadija aliyewakilishwa na Afisa Tarafa ya Mkuranga Ndg. Clement Muya alisisitiza utunzaji wa Mche ya miembe iliyopandwa sambamba na mizinga ya Nyuki iliyotolewa na Kampuni ya SONGAS ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali zinazohamasisha wananchi kufuga nyuki kisasa ili kuwa na ufugaji bora wa nyuki na kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na nyuki.
Akizungumzia umuhimu wa Sensa Bi. Hadija amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na makazi ifikapo Agosti 2022 huku akifafanua umuhimu wa zoezi hilo katika upangaji wa mipango ya maendeleo na ugawaji wa Rasilimali kwa wananchi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya na Diwani wa kata ya Shungubweni Mh. Shaibu Kambwili amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Bi. Mwantum Mgonja kuzungumza na walimu na kutenga mda wa kuwafundisha watoto wa shule za Msingi somo la ufugaji wa nyuki na kuwaeleza fursa zinazotokana na mdudu huyo ili kuwajengea uwezo na kuwapa ari ya ufugaji wa nyuki na utunzaji wa Mazingira wakiwa katika umri mdogo.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa ugawaji wa vifaa vya ufugaji nyuki ikiwemo mizinga na vifaa vya kujikinga na utunzaji wa nyuki kwa vikundi vinne vya wajasiliamali, na shule za msingi nne.
"Nyuki ni uchumi tuwalinde na kuhifadhi mazingira yao".
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.