NAIBU Waziri wa Mawasiliano na TEHAMA, Mhandisi Kundo Mathew, amekipongeza Kiwanda cha Raddy Fibre Solution kilichopo Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani kwa kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo juzi baada ya kukagua uzalishaji wa bidhaa za Mkongo wa Taifa unaofungwa na kiwanda hicho cha wazawa, Kundo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi, alisema uwekezaji huo uliogharimu sh.bilioni 1.7 utafanikisha ujenzi wa mkongo wa Taifa upungue gharama na kuokoa fedha za kigeni.
Mhandisi huyo alizitaka Idara za Uhamiaji na Zimamoto kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ili waweze kutimiza malengo yao kwani kiwanda hicho kitatoa ajira zisizopungua 400 sambamba na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya na Serikali Kuu.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Ramadhani Mlanzi, aliipongeza Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwezesha kuanza ujenzi, huku akiweka bayana azma yake ya kutengezeza cable za fibre kilometa 24 elfu kwa mwaka na kuongeza wao ni kati ya nchi tatu pekee za Afrika zinazofanya uzalishaji huo.
Katika taarifa ya Halmashauri hiyo iliyosomwa na Mkurugenzi, Mhandisi Mshamu Munde ilisema mazingira rafiki kwa uwekezaji ikiwemo ardhi ya kutosha imewavuta zaidi ya wawekezaji 80 hali iliyochangia kutoa ajira kwa wananchi na kupaisha mapato.
Akiwasilisha taarifa ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCSAF) Mkuu wa uendeshaji Albert Richard alisema wametumia sh.bilioni 161 za serikali kujenga mikongo kwenye Kata 1057 nchini huku Wilaya ya Mkuranga wakitumia milioni 200, ambapo Naibu Waziri aliridhika na usikivu baada ya kukagua.
Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Wilaya hiyo, Filberto Sanga aliwataka wajenzi wa mikongo kutoa taarifa kabla kwa Mkurugenzi, Uongozi wa Kata na Vijiji ili kujiridhisha zaidi kiusalama.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.