Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mh.Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile amewataka wananchi kuepuka magonjwa yasiyoambukizwa kwa kufanya Mazoezi, kula Lishe bora,kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi na matumizi ya tumbaku.
Dkt Ndugulile aliyasema hayo hapo Jana wakati wa ufunguzi wa huduma ya Macho,Kisukari na Shinikizo la damu Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ambapo huduma hiyo ilifadhiliwa na Lions Club ya Dar es Salaam,Kiwanda cha Knauf Gypsum Ltd kilichopo Mkuranga na Hospitali ya Regency iliyopo Dar es Salaam ambapo huduma hiyo ya matibabu ya bure ilianza tarehe 27.10.2017 na inatarajia kumalizika Leo hii tarehe 29.10.2017
Ndugulile alisema kwamba takwimu za Shirika la Afya zinaonesha kwamba jumla ya watu mil 253 wana matatizo ya kuona na wengi wao wanatoka kwenye nchi zilizoendelea na maskini ikiwemo Tanzania.
Aidha takwimu zinaonesha kwamba ifikapo 2030 vifo vitokanavyo na kisukari vitaongezeka maradufu ulimwenguni kote,takwimu pia zinaonesha Shinikizo la damu linaongoza bara la Afrika kwa asilimia 46 ikilinganishwa na asilimia 35 katika bara la America lenye idadi chache katika Shinikizo la damu.
Hata hivyo inakadiriwa takribani asilimia 1 ya watanzania wana ulemavu wa kutoona na asilimia 4 wana upungufu wa kuona ambapo asilimia 80 ya visababishi vya magonjwa hayo ni vile ambavyo vinaweza kutibika au kuepukika kama vile mtoto wa jicho.
Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na Taasisi ya NIMRI utafiti ulofanyika 2015 inaonesha viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yameonesha kuongezeka na kufanya idadi ya watanzania wenye tatizo la Shinikizo la moyo takribani asilimia 25.9 na kisukari asilimia 9.1.
Ndugulile alisisitiza kwamba kutokana na changamoto ya magonjwa hayo inahitajika juhudi za makusudi kwani magonjwa yasiyoambukizwa ni magonjwa ya muda mrefu na matibabu yake yana gharama kubwa hivyo ni vema kwa pamoja Serikali na Sekta binafsi kufanya kazi ya ziada ya kupambana na janga hili ambalo visababishi vyake vikubwa ni aina ya maisha tunayoishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Knauf Gypsum Ltd Georgios Zachopoulos alisema huduma hii ya matibabu itakua inafanyika kila mwaka kiwandani hapo kwa lengo la kuisaidia Jamii wenye matatizo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh Filberto Sanga alitoa shukrani za dhati kwa uongozi wa kiwanda cha Knauf,Lions Club ya Dar es Salaam na Hospitali ya Regency kwa moyo wa uzalendo.
Sanga aliongeza kwamba "tuna viwanda 54 na Sera yetu ni Uchumi wa Viwanda katika muitikio huu ndicho kilichofanyika leo ni matunda ya uwekezaji na Kiwanda cha Knauf walienda mbali zaidi kwa kukutana na uongozi wa Lions Club ya Dar es Salaam kwa lengo la kufadhili matibabu ya Macho, kisukari na Shinikizo la damu kwa siku tatu wananchi wa Mkuranga wamepata fursa pekee kwa kupata matibabu bure.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.