Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Abdallah Hamisi Ulega (Mb) ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kushirikiana na wananchi kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya na Watendaji wa Halmashari ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani alisema tatizo la wakulima na wafugaji ni changamoto kubwa, hivyo ni muhimu kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili mifugo yao isizagae hovyo.
“Tunahitaji tutenge,tupime na kumilikisha ardhi kwa ajili ya wafugaji, hii ni changamoto tunayotakiwa kuifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kudhibiti mifugo isizagae hovyo” alisema.
Aidha alisema kuwa Halmashauri inatakiwa kukagua, kupima ardhi, na kutengeneza miundo mbinu bora kwa ajili ya wafugaji na kuwapeleka huko. Alisema, kwa kufanya hivyo itarahisisha kuwatambua wavamizi na wasio fuata sheria na kuweza kuwashughulikia ipasavyo kwa mujibu wa Sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh Filberto Sanga alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa Mkuranga ni uuzaji wa ardhi, wananchi wanauza ardhi kiholela kiasi kwamba wanakosa maeneo ya kilimo hivyo amewataka wananchi kutouza ardhi hovyo.
Sanga alisema kuwa agizo la Naibu waziri wamelipokea ijapokuwa wana uhaba wa ardhi lakini wameainisha baadhi ya maeneo yaliyopo tarafa ya Mkamba ambayo watayafanyia ukaguzi kwa ajili ya wafugaji.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.