Maonyesho ya sherehe za wakulima na wafugaji Nane Nane ya Kanda ya Mashariki yamezinduliwa leo tarehe 1.08.2017 katika uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,Nanenane ambapo mgeni rasmi wa sherehe hizo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa Majaliwa lakini aliwakilishwa na Pro.Jumanne Maghembe (MB) Waziri wa Maliasili na Utalii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkoani Morogoro Prof Maghembe alisema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 Tanzania inakuwa na uchumi wa kati na mpaka sasa imebaki miaka nane ili nchi iwe Taifa lenye uchumi wa Kati na dhana hii lazima itekelezwa kupitia kilimo.
Prof Maghembe aliongeza kwa kusema nchi ya viwanda huenda sambamba na nchi ya kilimo kwani viwanda kwa asilimia tisini hutegemea malighafi kutokana na kilimo na maligafi za kilimo lazima zizalishwe za kutosha ili taifa litoke kwenye umaskini kwenda kwenye nchi wa uchumi wa kati.
“Ili wakulima wazalishe lazima wasikilize ujumbe mzuri wa bei ya mazao, kuwe na bei inayosimamiwa na serikali na bei inayolingana na bei ya soko la dunia, hatuwezi kufika taifa la uchumi wa kati bila kuwa na bei stahiki ya mazao. Pia wakulima wasimamiwe, wafuate misingi ya sayansi na teknolojia katika kulima ili wapate mazao mengi”.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng.Evarist Ndikilo alimshukuru Prof Maghembe kwa kutumia muda wake na kushiriki maonyesho ya Nanenane kanda ya Mashariki na alisema”kanda ya mashariki inakua siku hadi siku katika Nyanja za uzalishaji wa mazao ambapo Morogoro inaongoza lakini pia kwa upande wa viwanda Pwani na Dar es salaam ina viwanda vya kutosha hivyo hatuna shaka 2020 kwenye pato la taifa litaongezeka”
Maonyesho ya sherehe za wakulima na wafugaji Nane Nane ya Kanda ya Mashariki yameshirikisha Mkoa wa Pwani, Morogoro,Dar es salaam,na Tanga na Maonyesho ya mwaka 2017 yameambatana na kauli mbiu isemayo”Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo,Mifugo na Uvuvi ili kufikia uchumi wa kati”.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.