Maonyesho ya sherehe za wakulima na wafugaji Nane Nae kanda ya Mashariki yalifanyika Mkoani Morogoro katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikuhusisha Mikoa ya Pwani, Tanga,Dar es salaam na Morogoro ambapo kwa mwaka huu Maonyesho hayo yaliendana na kauli mbiu isemayo “Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati”.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo Mkoani Morogoro Bi Rither Barbaydu ambaye ni Mratibu wa Maonyesho ya Nane Nane Wilaya ya Mkuranga alisema maonyesho ya nanenane kwa mwaka 2017 yameleta mafanikio makubwa kwa wakulima na wajasirimali kwani bidhaa nyingi walizokuja nazo kwenye maonyesho zilipendwa sana na wananchi waliofika kwenye banda la Mkuranga walinunua bidhaa mbalimbali kama unga wa muhogo,unga wa viazilishe, korosho, bidhaa za usindikaji na bidhaa za ususi.
Bi Honoratha Mdichei mkulima katika wilaya ya Mkuranga kijiji cha Bigwa ambaye anajishugulisha na kilimo cha pilipili hoho,nyanya,na mbogamboga alisema kupitia maonyesho ya Nanene amejifunza vitu vingi,ikiwemo mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula na biashara.”zamani nilikuwa navuna mazao na yakibaki yanaharibika lakini kwa sasa nimefundishwa namna ya kusindika na hivyo nahifadhi chakula kwa muda mrefu pasipo kuhariba”
Bi Honoratha aliendelea kusema kwamba yeye ni mkulima ambaye anafuata taratibu zote za kilimo ili aweze kupata mazao mengi,ikiwemo kupalilia kwa wakati, kuweka mbolea kwa wakati na kumwagilia maji mengi ya kutosha pale yanapohitajika.
Bi Janeth Mbwambo Meneja wa Mkuranga Cassava Cooperative Joint Enterprises (MKUCACOJE)alisema katika maonyesho ya Nanenane wameleta bidhaa za unga wa muhogo,Unga wa Viazilishe na bidhaa zinazotokana na muhogo na viazilishe. ”Wateja wengi walipenda na walinunua kwa wingi na wengine walitoa oda na hivyo kusadia kupata masoko kirahisi kupitia maonyesho ya Nane nane”.Bi Janeth alisema
Aidha bi Janeth aliendelea kusema unga wa viazilishe ulikua kivutio kikubwa kwenye maonyesho hayo kwani wateja waliweza kuona na kuonja bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kupitia viazilishe ikiwemo juisi, uji, keki,maandazi,tambi na kripsi.
Katibu Tawala Wilaya ya Mkuranga Dk.Severine Lalika alisema maonyesho ya Nane nane kwenye banda la Mkuranga yamekuwa hai zaidi ikizingatiwa wakulima waliandaliwa vizuri kwa kutoa maelekezo kuanzia upatikanaji wa mbegu hadi upatikanaji wa bidhaa husika.
Dk Lalika alitoa ushauri kwa maonyesho yajayo jengo liboreshwe vizuri zaidi kwani kwenye maonyesho haya lengo ni kufanya biashara na kutafuta masoko hivyo jengo likiboreshwa wateja wengi watapata hamasa ya kuingia kwenye banda la Mkuranga na hatimaye kuitangaza wilaya ya Mkuranga.
Maonyesho ya sherehe za wakulima na wafugaji Nane Nane kanda ya Mashariki yalifanyika Mkoani Morogoro kuanzia tarehe 01-10/08/2017 yalifunguliwa na Prof.Jumanne Maghembe (MB) Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa Majaliwa na kwenye kilele chake yalihitimishwa na Dr.Hamisi Kigwangwala ambaye alimuwakilisha Makamo wa Raisi Mh. Samia Suluhu Hassan.Aidha Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imeshika nafasi ya pili katika Mkoa wa Pwani kwenye maonyesho hayo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.