Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga akiwakilishwa na Afisa Tarafa ya Mkuranga Clement Muya amevitaka Vikundi vitakavyonufaika na Mikopo ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kurejesha fedha hizo kwa wakati ili na wengine waweze kukopa .
Muya ameyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya ujasiriamali kwa vikundi vinavyotarajiwa kupata Mkopo wenye thamani ya Shilingi Milioni 63,690,000 kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga.
“Lengo la Mikopo hii ni kuondoa umasikini kwani sisi wenye vipato vya kawaida ni ngumu kupata Mikopo katika taasisi kutokana na matakwa ya taasisi hizo, ndiyo maana Serikali imeamua kutoa Mikopo hii katika makundi hayo” Alisisitiza.
Afisa Mikopo kutoka CRDB Devid Kaishe amewataka wajasiriamali hao kutumia fedha hizo kwa makusudio yaliyoandikwa kwenye andiko la Mradi sambamba na kuacha kuchukua mikopo hiyo kwa ajili ya kujifunzia Biashara.
Pamoja na hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira Hassan Dunda ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mkamba amewataka wataalam ngazi ya Wilaya kuvitembelea vikundi hivi mara kwa mara baada ya kupata mikopo ili kuona ni namna gani wameweza kuzitumia feda hizo sambamba na kuendelea kuwapa elimu kila mara.
Nae Afisa wa Benki ya NMB Halima Nkya kwa upande wake amewakumbusha wajasiriamali hao kuendelea kuitumia NMB pamoja na kutunza akaunti zao kwa makusudi ya kuzifanya akaunti hizo kuwa hai.
Mikopo hiyo ni takwa la Serikali la kutenga 10% ya Mapato ya ndani ya kila Halmashauri na kuzitoa kwa Makundi ya wajasiriamali kwa wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.