Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Afya) Profesa Tumaini Nagu ameipongeza Mkuranga kujenga Hospitali mpya na ya kisasa inayotoa huduma za maabara kwa kiwango cha kimataifa.
Hayo ameyasema tarehe 4 Mei 2025 alipofanya ziara ya siku moja ya kutembelea kituo cha Afya Kisiju na Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.
Profesa Nagu amesema Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika kuboresha miundo mbinu ya Afya ila kwa Mkuranga amejionea maabara nzuri na ya kisasa na inatoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu sana.
Aidha katika kuboresha huduma za Afya ameagiza zoezi la utoaji wa huduma za chanjo katika Hospitali ya Wilaya liwe la kila siku na muda wote sambamba na kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga jengo jipya la dharula (EMD).
Amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kufanya tathmini na kuona maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya Afya Nchini pamoja na kusikiliza kero na maoni kwa wananchi ili Serikali yao iweze kuzifanyia kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Awali akizungumza na watumishi katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri Nagu amesema maeneo yatakayofanyiwa tathmini ni pamoja na hali ya utoaji wa huduma katika vituo vya Afya na Hospitali, upatikanaji na matumizi sahihi ya Dawa, matumizi ya majengo na vifaa vya kutolea huduma, usimamizi wa fedha pamoja na huduma na chanjo na lishe.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mkuranga Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mohamed Mwera amemshukuru Mh. Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupatikana majengo mpya na ya kisasa na kuahidi kuyatumia vizuri majengo ya Hospitali hiyo kwa kupata huduma za Afya sambamba na kuilinda miundo mbinu hiyo.
Majengo mapya ya Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga yamejengwa kupitia fedha kutoka Serikali kuu na jumla ya Shilingi Milioni Mia tisa 900,000,000 zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi huo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.