Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amepongeza juhudi za Wilaya ya Mkuranga katika sekta ya uwekezaji kwenye Utalii zinazoendelea kufanyika katika kijiji cha Mpafu kata ya Dondo wilayani Mkuranga.
Ndikilo alisema hayo hapo jana wakati alipotembelea eneo la utalii lililopo kijijini hapo liitwacho Palacha Dream City linalomilikiwa na Zainnudin Adamjee kupitia kampuni ya Global land solution ambao ndio waendelezaji wa mradi huu ambapo kwa sasa wameshakamilisha mgawanyo wa matumizi ya ardhi ikijumuisha hoteli, nyumba za makazi, masoko, shule, maeneo ya biashara na huduma za kijamii.
“ kuanzisha jambo hili itakua tumefungua Utalii katika kanda ya kusini “Southern Circuit” kwani utalii kwa kanda hii bado haujaendelezwa sana lakini juhudi kama hizi za Global Land Solution zikiendelezwa zitaleta mchango mkubwa sana kwa jamii na Taifa kwa ujumla.”Ndikilo alisema
Ndikilo alisisitiza kwamba Pwani ina mwambao wa bahari ya hindi kwa takribani kilomita 300 zenye fukwe nzuri, mchanga mzuri, na kwa Palacha Dream city ina kilomita 4 yenye fukwe ndio maana wamepatikana wawekezaji kutoka Dubai na Hispania ambao watashirikiana na Global land solution kuendeleza Palacha Dream City.
Mkurugenzi Mtendaji wa Global land Solution bwana Zainuddin Adamjee alisema “Tutashirikiana na kampuni ya Dubai iitwayo Fahkrudin Properties ambao wamebobea katika ujenzi wa miradi kama hii duniani na kampuni ya Barcelo Group ya nchini uhispania ambao ni mabingwa wa uendeshaji wa hoteli”.
Adamjee aliongeza kwamba kuna changamoto mbalimbali zinazokabili mradi huu ikiwamo Mawasiliano ya simu hafifu, Maji na Umeme kwani unahitajika umeme mwingi kuanzia wakati wa ujenzi wa mradi hadi katika uendeshaji, pia ameomba uboreshaji wa barabara ya Mkuranga kwenda Kisiju ili iweze kuhimili mzigo wa tani 30 na pia barabara ya kutoka Dondo hadi Palacha iunganishwe katika mipango ya barabara hiyo.
Wakijibu changamoto hizo, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Regina Mvungi alisema REA awamu ya tatu italeta umeme mpaka kijiji cha mpafu ambapo itakuwa mwezi machi mwaka huu na ndani ya awamu ya tatu kuna hatua tatu, ambapo kwenye hatua ya pili umeme utafika hadi kwenye eneo la mradi wa utalii Palacha Dream City.
Kuhusu changamoto ya mawasiliano Meneja wa TTCL kanda ya kusini bwana Ramadhani Mshana alisema kutokana na changamoto hii kampuni yao ina mradi wa uwezeshaji mawasiliano vijijini (UCSAF), lakini kwa sasa wanaweza kutatua changamoto hiyo kwa kutumia satellite broadband ambayo itasaidia kwa kipindi hiki wakati wanaendelea kutafuta suluhu ya jambo hili.
Pia Kuhusu Changamoto ya maji, Meneja DAWASCO kutoka Kibaha bwana Grossman Makere alisema “kwa kuwa tayari walishaanza utaratibu wa kutatua changamoto hii ni vema watupatie andiko la mradi ili tuweze kufanya hatua za haraka”
Mhandisi Peter Shirima Meneja wa TARURA Wilaya ya Mkuranga alisema “Hatukuweka kwenye bajeti ya 2017/2018 na pia kwenye mapendekezo ya bajeti ya 2018/2019 ambayo imeshawasilishwa lakini tutaiandikia andiko wiki hii na kufanyia upembuzi ili tupeleke maombi maalum Wizarani ili tuone kama tunaweza kusaidiwa.
Katika hatua nyingine wakati akitembelea kiwanda cha Lodhia Steel and Plastic Company Limited, Mhe. Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kutambua Viwanda ambavyo vimekamilika vinavyohitaji kufunguliwa rasmi na viongozi wa juu wa Serikali, ambapo alitaja kuwa viwanda tisa vimekamilika vinavyohitaji ufunguzi huo, viwanda hivyo ni:-
Twyford Ceramic Company Ltd kiwanda cha vigae, KEDS washing Powder kiwanda cha sabuni , Jafra Investment & Suppliers Ltd Mabomba yaPlastiki, Budget Movers Co. Ltd kiwanda cha kuunganisha mabodi yamabasi na Hunan Power Group kiwanda cha Nguzo za zege, Sayona Fruit Processing Plant kiwanda cha kusindika Matunda, na viwanda vitatu vya Lodhia steel anda plastic vinavyozalisha nondo, bomba na plastiki.
Aidha, alitaja faida za kiwanda hicho ni pamoja na kujenga barabara inyoingia kiwandani hapo, ajira zaidi 1500 walizotoa kwa watanzania mchango wao wa mapato kwa serikali.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.