Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng.Evarist Ndikilo amewajia juu baadhi ya vyama ya Msingi vya Mkoa wa Pwani kwa kuhujumu mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuchanganya mawe na mchanga kwenye korosho .
Ndikilo aliyasema hayo hapo jana kwenye kikao cha wadau wa Korosho Mkoa wa Pwani kilichofanyika Wilayani Mkuranga kwenye ukumbi wa Kiguza Flex.
Ndikilo alisema”Mkoa wa Pwani umechafuka kwa sababu baadhi ya vyama ya msingi kuchanganya mawe na mchanga kwenye korosho hivyo ni lazima kuwe na maamuzi sahihi kwani huu ni uhujumu uchumi, nchi yetu imechafuka kwa sababu ya watu wachache wanaoharibu ubora wa korosho na uzito kwa lengo la kutengenza fedha ya bure bila jasho,inabidi tutoke huko na tubadilike”
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Ndikio akihutubia katika kikao hicho, Kulia ni Mkuu wa wilaya Mhe. Filberto Sanga
Ndikilo aliongeza kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani upo ndani ya Ilani ya chama cha Mapinduzi lakini pia ni mfumo ambao umelenga kumkomboa mkulima wa hali ya chini hivyo wale watu wachache wenye lengo la kuhujumu mfumo huu serikali itawachukulia hatua za kisheria.
Ndikilo alisisitiza kwamba magunia ya Mkoa wa Pwani yana alama ya rangi ya kijani hivyo yahifadhiwe kwa uangalifuili yasiangukie kwenye mikono ya watu wahalifu ambapo yakichukuliwa na watu tofauti yanaweza kuwekewa korosho ambazo sio za Mkoa wa Pwani na kusababisha Mkoa huo kuchafuka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga Mh Juma Abeid alisisitiza kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani upo kisheria na hivyo hauwezi kupingwa na watu wachache na pia serikali haiwezi kupingwa kilichobaki ni utekelezaji tu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga Mh Juma Abeid akichangia mada katika kikao hicho
Rashidi Selungwi Mdau wa korosho kutoka Wilayani Mkuranga alisisitiza juu ya kuwasimamia viongozi wa vitongoji kwani hutoa takwimu za mikorosho ambayo si sahihi ”Tungekuwa na takwimu sahihi zingepatikana tani zaidi ya milioni 20 katika Mkoa wa Pwani”
Bei dira iliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa wadau wa Korosho kwa mwaka 2018/2019 ni daraja la kwanza Tshs 1550 na daraja la pili ni Tshs 1240.
Maandalizi ya msimu wa korosho 2018/2019 unaendelea vizuri kwani gunia 320,000 zimeagizwa na mzabuni Dirma Holdings Ltd kwa ajili ya kuwekea korosho za Mkoa wa Pwani na magunia hayo yataletwa kabla ya tarehe 09.10.2018.
Aidha matumizi ya Ghala kuu hadi sasa yamepitishwa maghala mawili ambayo ni ghala la Costantine Mumba-Mwanambaya- Mkuranga na Ghala la TANITA Kibaha.
Wadau wa zao la Korosho kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani wakifuatilia kikao
Aidha wadau wa Kikao hicho waliomba wapate ghala lingine kutoka Kibiti kutokana na umbali mrefu kutoka Rufiji hadi Mwanambaya Wilayani Mkuranga kwani pia umbali huo unaweza kusababisha korosho kutoroshwa na kuuzwa maeneo mengine kabla ya kufika eneo husika.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.