Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira Mhe Luhaga Mpina (MB) jana ameufunga mgodi wa mchanga unaomilikiwa na Christopher Lema uliopo katika kijiji cha Kolagwa kata ya Tengelea wakati alipokuwa kwenye ziara yake Wilayani Mkuranga.
Mpina alifikia maamuzi hayo baada ya kuona uharibifu mkubwa wa mazingira ambao umesababisha mmomonyoko wa ardhi kiasi cha kuhatarisha maisha ya wapita njia na hasa wanafunzi wanapoelekea shuleni.
Akiongea na wananchi waliojitokeza katika eneo hilo Mpina alisema, “Uchimbaji ulianza kiholela na haukuzingatia taratibu na Taasisi za Serikali yaani Halmashauri,NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira) na Wizara ya Nishati na Madini zilikosea ilibidi zijiridhishe dhidi ya uchimbaji wa ardhi na hatma ya wananchi wanaoishi eneo hilo,inavyoonesha hakuna mkutano wa kata wala kijiji ulioridhia kuhusu uchimbaji wa eneo hili.”
Mh mpina aliagiza ndani ya siku 14 Halmashari ya Wilaya ya Mkuranga, NEMC na Wizara ya Nishati ya Madini wafuatilie athari zilizojitokeza na kuangalia taratibu zote za uchimbaji kama zilifuatwa na ikigundulika taratibu hazikufuatwa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya makosa atayopatikana nayo ikiwemo kupigwa faini kulingana na athari zilizojitokeza au kurejesha mazingira katika hali ya awali.
Katika hatua hiyo pia Mpina alitembelea kiwanda cha Bakhresa na kujionea mazingira ya kiwanda hicho na kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo hilo juu ya kelele kutoka kwenye kiwanda hicho na pia maji ya mvua yanayotiririka na kuingia kwenye makazi ya watu.
Aidha Mpina ameagiza Taasisi za Serikali zinazohusika kupima kiwango cha sauti au kelele zinazosababishwa kwenye kiwanda hicho na pia kupima maji yanayotiririshwa kama yana viwango vilivyoruhusiwa.
Mpina aliongeza kwamba kama majibu yataonesha kelele zinazidi kwa mujibu wa kanuni za mazingira wataelekezwa kupunguza kelele hizo na maji kama ni machafu hawataruhusiwa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Mpina alifurahishwa na wananchi wa Mkuranga kwa upendo waliounesha wakati walipofika kwenye ziara yake na aliahidi kurudi tena wilayani Mkuranga ili kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.