Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema Serikali ya awamu ya tano imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 16.1 kuendeleza sekta ya Elimu ndani ya Mkoa wa Pwani kwa kipindi cha Miaka mitano.
Ndikilo ameyasema hayo jana akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Mkuranga wakati wa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi Chatembo iliyoko kata ya Mwandege ambayo imetengewa kiasi cha shilingi milioni mia nne (400) hadi kukamilika kwake.
Katika kuhakikisha kuwa Mkoa wa Pwani unatekeleza na kuunga Mkono juhudi za Mh. Rais John Pombe Magufuli katika sekta ya elimu Ndikilo amewaagiza Wakuu wa Wilaya ya Wakurugenzi wote wa Halmashauri kutokwenda Likizo hadi hapo watapohakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanakwenda shule.
Aidha akiwa katika ziara hiyo Ndikilo amewataka wamiliki wa kiwanda cha Saruji cha Rhino kilichopo Kisemvule kuacha mara moja kuhamisha vipuli vya kiwanda hiko kupeleka Mkoani Tanga hadi hapo watakapokaa pamoja na kuona ni namna gani itawafaa kufanya ili kutatua changamoto zilizopo na hatimaye Kiwanda hiko kiweze kuleta tija ndani ya Wilaya ya Mkuranga.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega amemuomba kumsaidia kufanikisha ukarabati wa Barabara kutoka Bakhresa kwenda chatembo pamoja na kuwekwa kwa umeme katika shule hiyo mara tuu itakapokamilika na hata changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili wilaya ya Mkuranga sambamba na kumuomba rais aje kuizindua shule hiyo itakapokamilika.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga amemshukuru Mh. Rais pamoja na Mkuu wa Mkoa sambamba na kumuunga Mkono Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kwa kuwasilisha vema changamoto za Jimbo la Mkuranga na kumuomba Mkuu wa Mkoa kutusaidia kwani hiko ndicho kilio cha wana Mkuranga.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alipata fursa ya kutembelea na kukagua majengo mapya 14 ya madarasa, jengo la Nyumba ya Mwalimu sambamba na jengo la utawala katika shule Mpya ya Chatembo, pamoja na kuzindua karakana ndogo ya kutengeneza Madawati katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.