Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Mh. Khadija Nasri Ali ametoa katazo la michango ya chakula mashuleni huku akiwataka wazazi, walimu na wataalamu wa lishe kuanzisha utaratibu wa mashamba ya chakula na bustani za mboga kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya njaa Mashuleni.
Akizungumza kwenye Mkutano wa baraza la Madiwani lililoketi kujadili taarifa za robo ya nne kwa mwaka wa fedha 21/22 Mkuu wa Wilaya aliwataka wataalamu wa lishe kuanzisha utaratibu wa kuwajengea vijana uwezo wa kujisimamia katika uzalishaji wa chakula kwani itawasaidia hata wanapomaliza elimu zao.
"Hatuwezi kuendelea na utaratibu wa kuchangisha wazazi michango ya kununua chakula ili hali tunao uwezo wa kuanzisha bustani za mboga mashuleni na kuwawezesha watoto wetu kupata chakula bila kuchangishana fedha"
Akiendelea Mh Nasri alisisisitiza kwa kusema nimegoma kutoa vibali vya kuchangisha kwa sababu nimeona haitusaidii kuwa na suluhisho la kudumu la changamoto hii.
Akizungumzia suala la ufaulu wa masomo Mh. Khadija aliwataka wazazi na walezi kusimamia nidhamu na uadilifu ili kuweza kukuza ufaulu wa vijana hao na kuweza kukabiliana na soko la ajira ambalo limelenga kutumia watu wenye elimu na ujuzi ku huku akisisitiza wawekezaji wa viwanda wamekua wakija kwa wingi hivyo kupelekea kuhitaji kuajiri watu wenye ujuzi na elimu ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Nchi.
"Niwaombe wazazi na walezi tuwe wasimamizi wazuri kwa Vijana wetu tuwafundishe maadili mema huku tukiwahimiza kusoma kwa bidii"Alisema.
Sambamba na hilo Mh Nasri amewaonya wazazi kuto shirikiana na wahalifu wanaofanya makosa ya kuharibu watoto matendo ya ulawiti na ubakaji kwa makusudi kwa kukaa nao meza moja na kujadili namna ya kuyafumbia macho makosa wanayoyatekeleza isipokua kushirikiana na jeshi la polisi kupinga vikali uhalifu huo.
Baraza la Madiwani lilichagizwa na uchaguzi wa Makamu mwenyekiti huku Mhe. Shomari Mwambala Diwani wa kata ya Kiparang'anda akiibuka mshindi kwa kupata kura 33.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.