TASAF awamu ya tatu-Mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani Mkuranga ulianza mwaka 2015 na unahusisha vijiji 77 kati ya 125 na jumla ya kaya 5,045 zilianza kupata ruzuku lakini hadi kufikia sasa kaya 4690 ndizo zinazopokea ruzuku. Kaya 355 zimeondolewa kwa sababu mbalimbali kama kuhama kutoka eneo la utekelezaji au kifo hivyo kukosa sifa za kuwepo kwenye mpango.
Madhumuni ya TASAF awamu ya tatu ni kuziwezesha kaya kupata mahitaji ya msingi na fursa za kujiongezea kipato na walengwa wa mpango ni kaya maskini katika maeneo yalioainishwa.
Hayo yalisemwa hapo jana na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mkuranga bwana Kudra Timoth wakati akiratibu zoezi la uhawilishaji katika kijiji cha Mbulani kata ya panzuo.
Kwa upande mwingine, Bwana Muharami Makutike Afisa Mtendaji kijiji cha Mbulani alisema mpango wa kunusuru kaya maskini umewasaidia wananchi wa kijijini hapo kwa mafanikio makubwa ikiwemo wengine kujenga nyumba za bati, wakina mama kujiunga kwenye vikundi na kufanya biashara ndogondogo na wengine kufungua migahawa
Alisema, “kwenye kijiji changu nina walengwa 115 na kati ya hao walengwa 28 wanalipwa kwa njia ya mtandao na walengwa 87 wanalipwa kwa njia ya fedha taslimu. Hali zao za maisha sasa zinaridhisha tofauti na ilivyokuwa awali; naipongeza serikali”
Bi Halima Ally mkazi wa kijiji cha matanzi kata ya Beta alisema “Naishukuru sana Serikali kwa kunisaidia kuingia kwenye mpango huu wa kunusuru kaya maskini kwani nilikuwa napata tabu mimi na familia yangu kwa kuishi kwenye nyumba ya makuti lakini kwa sasa nalala kwenye nyumba yenye bati.”
Mwenyekiti wa kijiji cha Matanzi bwana Ibrahim Mkenda anasema changamoto kubwa anayokutana nayo kwenye mpango huu ni baadhi ya wananchi kuonekana kuwa na makazi duni na kuingizwa kwenye mpango huu ingawa wana uwezo wa kupata fedha,vilevile kuachwa kwa baadhi wa wananchi wasiojiweza sababu ya kuwa ndugu zao wana uwezo wa kuwahudumia.
TASAF awamu ya tatu-Mpango wa kunusuru kaya maskini unawezesha kaya maskini umewezesha kaya maskini kupata mahitaji ya msingi, kulinda rasilimali zao na kuweka akiba kwa ajili ya kujiletea maendeleo na hatimae kijitoa kwenye umaskini.
Vilevile Mpango huu umesaidia kuleta mafanikio kwa walengwa na jamii kwa kupunguza vifo vya watoto na wazee na kupunguza utoro kwa watoto hawa walio katika kaya maskini. Pia walengwa wengi wamejiunga katika vikundi vya uzalishaji maji na kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaohudhuria shuleni na kwenye vituo vya afya
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.