MFUKO wa Maendeleo ya Jamii,Tasaf, umeziwezesha familia zilizokuwa na
kipato cha chini na makazi duni, kuzipatia kipato ambapo wameweza
kunufaika kimaisha kutokana na jamii kuwa na kipato duni na makazi duni hali hiyo
ilisababisha hata kushindwa kula milo mitatu na wengine kushindwa hata
kuwapeleka watoto shule kutokana na kukosa fedha za kujikimu na
kununua chakula cha milo mitatu.
Katika kukabilina na changamoto hizo, Mkuranga ni miongoni mwa Wilaya
ambazo wakazi wake wamenufaika na ruzuku kutoka Tasaf na hali hiyo
imewasaidia kuboresha makazi yao ikiwamo kula milo mitatu,kuwapeleka watoto shule ,kupata ajira na kuwapeleka watoto kliniki.
Hayo ni maneno ya mmoja wa wanufaika wa Tasaf anaelezea hali ya maisha
yake kwa sasa.
Halima Ally anasema yeye alikuwa akilala katika chumba kimoja
kilichoezekwa na majani na akiwa na watoto nane.
Anasema yeye ni mkazi wa kijiji cha Matanzi Kata ya Beta Wilaya ya
Mkuranga Mkoani Pwani, anasema chumba hicho ndicho alichokuwa akiishi
na watoto wake nane na humohumo ndipo alipokuwa akipikia.
Anasema aliingizwa katika tasaf mwaka 2015 na amekuwa akilipwa kiasi
cha shilingi elfu 60 kila baada ya miezi miwili.
“Nilianza kulipwa fedha hizo sikuchezea maisha nilikuwa nanunua
mabati naweka na mpaka nilipoweza kujenga nyumba na kuiweka
mabati,’’anasema.
Anasema katika maisha yake amefanikiwa kupata watoto nane ni wawili
ambao wanasoma shule na wengine hawakuweza kuingia shule kutokana na
kushindwa kuwasomesha kwa kutokuwa na kipato.
Anasema kazi yake kubwa ni kuwalimia watu mabondeni ili aweze kumudu
maisha, lakini pamoja na kilimo hicho cha kuwalimia watu hakuweza
kubadilisha maisha yake kama ilivyo kwa sasa baada ya kuingizwa
Tasaf.
Anaongeza kuwa anaishukutu sana Tasaf ambayo imeona hali ya maisha
yake na kuyabadilisha na kumfanya leo analala katika nyumba iliyobora
na salama.
Juma Rashid ambaye ni mume wa Halima anasema kuwa, anaishukuru TASAF
kwa kuwaboreshea maisha yao.
Anasema awali walikuwa wakiishi katika chumba kimoja cha majani,
lakini leo hali yao ya maisha imebadilika na kuishi katika nyumba
iliyokuwa ya kisasa.
Afisa Mtendaji kata ya Beta, Ally Nassoro Mbalika anasema kuwa,
mpango wa TASAF katika kata hiyo umeingia mwaka 2015.
Anasema walengwa wamenufaika na fedha hizo, ambapo wapo walio nunua
mifuko, mabati na kutengeneza nyumba zao.
Anasema katika mafanikio hapakosi changamoto na kuongeza kuwa, kuna
baadhi ya watu ambao hawakuwapo katika mpango huo wa ruzuku, lakini
baada ya kukimbilia mjini na waliposikia watu wananufaika, wakarudi
vijijini na kutaka waingizwe katika mpango huo.
Anasema kuna utaratibu wa watu kupata fedha za ruzuku na sio kila mtu
ambaye anaingia kijiji anapata fedha bila ya kupitia taratibu na wale
wasiojua hilo, wanatoa malalamiko kuwa wameachwa kuingizwa katika
mpango huo.
Asha Kondo anasema TASAF imemsaidia kuboresha nyumba yake, kwa kuweka
mabati na kuongeza kuwa anapata kila miezi miwili elfu 44.
Mtendaji kijiji cha Mbulani Muharami Mwakitika anasema walengwa
katika kijiji chake wapo wanaorushiwa kwa njia ya mitandao na wapo
wanaopewa kwa njia ya kawaida.
Anasema katika kijiji hicho kuna watu ambao wamelipwa kiasi cha
shilingi milioni 6.7 kwa njia ya kawaida na kiasi cha shilingi milioni
10 kimelipwa kwa watu wa njia ya mtandao.
Anasema palipo na mafanikio napo hapakosi changamoto ambapo kuna
baadhi ya watu wamepoteza laini za simu na hali hiyo imekuwa
ikiwafanya wawapatie maelekezo ili kwenda kwa mawakala wapatiwe laini
zingine.
Anasema kuwa kuna baadhi ya walengwa ambao ni wazee wanaishi vijijini,
wanaingiziwa pesa, lakini kutokana na mtandao kusumbua wamekuwa
wakilalamikia kutopata pesa.
Anasema walengwa walionufaika na ruzuku, wameweza kununua mbegu na
kulima, wapo walianzisha migahawa,wapo walioboresha migahawa yao na
wapo walioboresha maisha .
Asma Magoma anasema TASAF imemwezesha kufuga kuku kwa kupatiwa elfu 44
pia watoto wanahudhuria masomo na kuongeza kuwa kibanda chake
kilichokuwa kinavuja sasa kakiwekea mabati.
Zakia Said Mkonge anasema yeye kafungua mgahawa kutokana na kupata
fedha kutoka TASAF.
Anasema awali alikuwa akipokea elfu 48,000 sasa anapokea elfu 42.
Kwa mujibu wa Mratibu wa TASAF Mkuranga bwana Timoth Kudra anasema kuwa,
zaidi ya shilingi bilioni mbili, zimetolewa kusaidia kaya masikini
kuboresha mfumo wa maisha.
Anasema hayo alipotembele katika vijiji mbalimbali na kuziona familia
ikiwamo na wengine kuchukuwa ruzuku.
“Wilaya ya Mkuranga ina vijiji 125, vijiji 77 vipo katika mpango wa
TASAF ambapo mpaka sasa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili,
kimetolewa kwa walengwa wanaonufaika na mfuko huo,’’anasema
kuwa mwaka 2014 walianza kwa kuibua kaya masikini, ambapo mwaka
2015 walianza na utekelezaji.
Anasema kaya 4,690 zimenufaika na ruzuku hiyo.
Anasema kuwa, Katika Wilaya ya Mkuranga, wanawalipa kaya masikini,
ruzuku ya msingi, na masharti.
Anasema katika ulipaji zaidi ya watu 3000 wanalipwa kwa njia ya
kawaida na zaidi ya watu 1900 wanalipwa kwa njia ya mtandao.
Anasema huo ni mzunguko wa 16, lakini katika ulipaji wa njia ya
mtandao kumekuwapo na changamoto ambapo baadhi ya watu kutokuwa na
vitambulisho vya kupigia kura na wengine kutojua kusoma na kuandika.
Anasema ruzuku imeboresha malengo ya walengwa.
Anasema kaya zilizokuwa zikipata mlo mmoja nazo ziliingia katika
vigezo vya kupata fedha.
Anaongeza kuwa utimizaji wa masharti unatakiwa kuzingatiwa Anasema
kama wazazi au walezi wasipopeleka watoto shule hao wakikuta kuna
changamoto katika malipo wanalalamika.
Mwisho.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.