Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amefanya ziara katika Kata ya Kisiju kwa kutembelea bandari ndogo ya Kisiju kujionea changamoto katika bandari hiyo pamoja na kukutana na Wazee wa Kisiju ambao wamemtuma awafikishie kilio chao kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Wakimsomea muhtasari wa Kikao maalumu cha wazee kilichowajumuisha Madiwani wa Kata ya Dondo na Kisiju kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Sotele juzi, wazee hao maarufu wamemwomba Rais wao ambaye ni msikivu na mtetezi kwa wanyonge ahakikishe anawaletea Barabara ya Lami kutoka Mkuranga hadi Kisiju Pwani kabla mauti hayajawakuta.
Wakiendelea kuwasilisha taarifa hiyo kwa Kiongozi huyo kwenda kwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa (CCM) Taifa, wazee hao wanaomba kushushiwa umeme katika baadhi ya Vijiji kwani pamoja na kutoa maeneo yao yakiwemo mazao lakini baadhi ya Vijiji vyao nishati hiyo tegemeo katika kuanzisha Miradi mbalimbali imewaruka na kubaki gizani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa (CCM) Wilaya ya Mkuranga Mzee Ally Msikamo aliungana na wazee wenzake kumsisitiza Mbunge wao awafikishie ujumbe huo kwa Rais kama ulivyo hatmaye kilio chao kipate ufumbuzi kwani wanasema tangu wazaliwe hadi umri unaelekea kuwaacha suala la kuwepo kwa barabara ya lami wanasikia kwa wenziwao tuu huku wakiweka bayana umuhimu wa Barabara hiyo kwamba ni muhimu kwa kuwa inapitisha korosho zaidi ya tani elfu kumi kila mwaka sambamba na fursa ya uwekezaji kwenye fukwe mbalimbali.
Naye Mbunge Ulega baada ya kupokea Muhtasari huo aliwahakikishia kuwa mambo yote atayafanyia kazi sambamba na kuwasilisha maombi yao hayo kwa Rais, lakini pia amewaambia wazee hao kuwa suala la bandari atalisimamia kwa kadri ya uwezo wake ili isife kwani anajua umuhimu wa Bandari hiyo kwa wananchi wa Kisiju na Halmashauri kiujumla.
Aidha aliwataka wananchi wote ambao hawajalipwa fedha zao za Korosho kuandika majina yao na taarifa zao aweze kuwasaidia ili kila mmoja awe kukamilisha mipango yake ukizingati tayari msimu mpya wa zao hilo umeanza.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.