Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Khadija Nassir Ali amewataka watumishi wote hasa wale wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoa huduma kwa vikundi vinavyoomba mkopo wa 10% kwa weledi.
Agizo hilo amelitoa Septemba 19, 2024 akiwa katika hafla ya utoaji wa Mikopo hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Stendi kuu ya mabasi Wilayani humo.
"Hakuna mtumishi hana mshahara, kika mtumishi ana mshahara wake, tumewekwa katika nafasi mbalimbali kwenda kuwatumikia watanzania, kwenda kuwatumikia wananchi wa Mkuranga, leo hii wananchi wanafika katika ofisi zetu wakiwa wanataka msaada na sisi baada ya kutoa msaada tunakwenda kuwarudisha nyuma" alisisitiza.
Amesema suala la Mikopo linahitaji nidhamu ya hali ya juu ili kuunga mkono jitihada za Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa yeye tayari ameshakamilisha kazi yake ya kutoa fedha hizo, hivyo jukumu lililobaki ni kutumia fedha hizo vizuri na kuzirudisha kwa wakati ili wengine waweze kupata Mikopo hiyo.
Aidha amewataka maafisa maendeleo ya jamii Kata zote kuhakikisha wanakwenda kuvisimamia vizuri vikundi vyote vilivyochukua mikopo kuwatembelea kila mara na kuona changamoto ili kuweza kufanikisha vikundi hivyo kurudisha mikopo hiyo kwa wakati.
Amesema mikopo hiyo ya 10% haina chama, haina itikadi ya Dini wala Kabila bali mikopo hiyo itaangalia sifa zilizoainishwa na kama unazo mikopo utapata.
Akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mkuranga Mwanansiu Dossi amesema kwa kipindi hiki cha robo ya kwanza ya Mwaka 2024/25 jumla ya vikundi vinne vimekidhi vigezo na kupewa jumla ya Shilingi Milioni 94.9.
Mkuranga imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 2.1 kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.