Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Filberto Sanga amezindua rasmi jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi wilayani Mkuranga hapo jana ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama samia Suluhu Hassan kuwa kila Wilaya iunde jukwaa la wanawake.
MKuu wa Wilaya huyo alisema kwamba dhumuni la kuunda jukwaa hili katika wilaya ya Mkuranga ni kuwapa fursa wanawake wa wilaya ya Mkuranga kukutana pamoja na kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo yao hasa fursa na changamoto wanazokumbana nazo katika suala zima la maendeleo ya kiuchumi na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli zingine za kiuchumi, hivyo kupitia jukwaa hili wanawake watapata fursa zilizopo katika wilaya hii ikiwemo viwanda vikubwa na vidogo vinavyozalisha bidhaa mbalimbali ambavyo ni soko la malighafi na fursa ya ajira.
Aliendelea kusisitiza kwamba jumla ya viwanda 57 vimeanzishwa katika wilaya ya Mkuranga hadi sasa.Vilevile Wilaya ina ardhi yenye rutuba na bora kwa mazao kama mihogo, matunda, korosho ambayo ni fursa kushiriki katika kilimo cha biashara ili kukuza uchumi wa Mkuranga.
Mkuu wa Wilaya huyo pia ameliagiza jukwaa hili kukutana kila baada ya miezi sita kwa kufanya vikao vyake na kuwasilisha taarifa za vikao katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na ofisi yake ili kujua kitu gani kinaendelea katika jukwaa hilo, lakini pia aliwaagiza waratibu wa uwezeshaji ngazi ya kata kuhakikisha wanaunda majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika kata na kuwasilisha taarifa hizo kabla ya Novemba 30 2017.
Mwenyekiti wa Jukwaa hilo bi Mariama Ulega aliwashukuru wakina mama wa Mkuranga kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo na aliahidi kufanya kazi kwa uwezo wake wote bila kujali itikadi ya chama, dini wala kabila na kuhakikisa wanawake wa Mkuranga wanasonga mbele.
Mratibu wa Jukwaa hili Bi Sylvia Gordon ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii alitoa rai kwa Taasisi za kifedha na mashirika mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati pamoja na huduma stahiki bila vikwazo na urasimu wowote ili kuwarahisishia kujukwamua kiuchumi.
Wanawake wamekuwa hawapati fursa za kutosha za kiuchumi hapa Tanzania na duniani kote,Hivyo Taifa limeona kuwa ushiriki wa wanawake katika shughuli za uchumi ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yetu na jamii kwa ujumla kwa sababu ushiriki wa mwanamke katika uchumi unalete mabadiliko makubwa sana katika uchumi wa familia na jamii kwa ujumla.
Katika harakati za kufikia malengo endelevu ya 50/50 ifikapo 2030 ambayo pia yanasisitiza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katibu wa umoja wa Mataifa aliteua timu ya viongozi na wataalam watakaofanya kazi kama chombo cha kutambua na kuweka mikakati ya kupunguza na kuondoa pengo kubwa ambalo limejengeka duniani sambamba na kuongeza ushiriki wa wanawake katika kukuza uchumi ili kurekebisha hali iliyopo sasa.Katika timu hiyo Mheshimiwa makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mjumbe.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.