Vijiji 79 kati ya 125 (Sawa na asilimia 63) vimepatiwa umeme katika mpango wa REA 3 mzunguko wa pili Wilayani Mkuranga.
Katika maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa REA Tanzania Bw. Hassan Saidi leo Machi 15, 2022 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji miradi ya Umeme Mbele ya Waziri wa Nishati Mh January Makamba aliyeongozana na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa lengo la kutembelea na kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa na REA katika Vijiji vya Mangombe, Mikere na Ngarambe vilivyopo kata ya Njia Nne Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Bw. Said alisema kuwa vitongoji vilivyopatiwa umeme ni 211 kati ya 476 Sawa na asilimia 44.
Mkuu huyo alifafanua kuwa tayari vitongoji 265 kati ya 476 sawa na asilimia 56 bado havijaunganishiwa umeme na kuwa kati yao vitongoji 44 vitapatiwa umeme katika mradi wa REA3 mzunguko wa pili unaoendelea kutekelezwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Bi. Hadija Nasri Ali aliwasilisha ombi lake Mbele ya Waziri Makamba na Kamati ya Bunge ya Nishati kuwa kituo cha kufulia umeme kijengwe ndani ya Wilaya hiyo ambayo kwa sasa inao uhitaji mkubwa wa Umeme kutokana na ongezeko la Viwanda.
Wakitoa neno la shukrani mbele ya Waziri Makamba na Kamati ya Bunge, Omari Makumbatu na Ashura Mongo wote wakiwa ni wakazi wa Kijiji cha Mikere wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea huduma za umeme karibu na kuwawezesha wazee kupata matibabu nafuu katika vituo vya afya sambamba na upatikanaji wa dawa za uhakika.
Nae Diwani wa kata ya Njia Nne. Ally Mambo ameiomba serikali kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha kuunganisha umeme katika Vijiji vilivyobaki ndani ya kata hiyo.
Kazi ya kusambaza umeme Vijijini katika Mradi wa REA awamu ya Tatu mzunguko wa pili katika wilaya ya Mkuranga inatekelezwa na mkandarasi China Railway Construction Electrification Bureau Group (CRCRBG) ambaye kwa sasa anaendelea na usimamishaji wa nguzo na kufunga waya kwenye maeneo mbalimbali Vijijini ambapo hadi sasa tayari mkandarasi amekamilisha ujenzi wa miundo mbinu ya kusambaza umeme katika vijiji saba (7) ambavyo ni Mponga, Mikere, Mingombe, Mamdimpera, Mamdimkongo Makumbea na Misasa katika wilaya ya Mkuranga.
Ujenzi katika Vijiji vya Kikundi na Kikoo utakamilishwa ndani ya mwezi machi, 2022 na Mradi huu ni wa miezi 18 na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2022
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.