Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bwana Peter Nambunga amewataka viongozi wa vyama vya ushirika Wilaya ya Mkuranga Kufuata mfumo wa stakabadhi ghalani katika mafunzo yaliyofanyika leo kwa viongozi hao katika Wilaya ya Mkuranga.
Nambunga alisema kufanyika kwa mafunzo hayo ni sehemu muhimu katika kuhakikisha wako tayari kuingia katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani”Ifahamike kuwa viongozi wa vyama vya ushirika wanalo jukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa mnamkomboa mwanachama na mkulima ambaye si mwanachama kwa kukusanya korosho zilizo bora ambazo zitakuwa zimedarajishwa kutoka kwa mkulima ili zipelekwe kwenye ghala la mnada tayari kwa kungojea wanunuzi wanunue korosho zetu”alisema Nambunga
Nambunga aliongeza kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kujua muongozo namba moja wa Bodi ya korosho ambayo inajumuisha majukumu ya viongozi wa vyama vya ushirika katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani na kupitia mikataba yenye tija kwa watendaji wa vyama vya ushirika.
“Natambua kuwa kuna baadhi ya vyama havijakamilisha taratibu za kisheria,baadhi yenu mmeshindwa hata kurudisha mrejesho kwa wanachama wenu kutokana na shughuli mlizosimamia msimu uliopita”Nambunga alisema.
Afisa Ushirika Wilaya bwana Valentine Shija alisema “Msimu wa 2017/2018 vyama vya ushirika 44 vilifanya kazi ya kukusanya korosho za wakulima,kati ya hivyo 26 tu ndio vilikamilisha taratibu za kisheria ili viweze kufanya kazi msimu wa 2018/2019”.
Shija aliongeza kwamba vyama vilivyobaki vilikuwa na baadhi ya changamoto ikiwemo kutokuwa na uongozi au idadi pungufu iliyotokana na kujiuzulu baadhi ya vongozi na wengine kusimamishwa,kutokuwa na watendaji wenye sifa au baadhi ya wajumbe wa bodi kufanya kazi za makatibu jambo ambalo limepelekea kuwepo na migogoro au kutokamilisha majukumu ya chama kwa ufanisi.
Shija alisisitiza kwamba “Mikakati ya kutatua changamoto hizi inaendelea kupitia usimamizi wa mara kwa mara,kaguzi za ndani na nje na kuvipa muda vyama ambavyo havina vigezo kujiandaa ili msimu wa 2019/2020 viwe vimekamilika kufanya kazi za chama”.
Mrajisi Mkoa wa Pwani Angela Nalimi alisema hapo awali kulikuwa hakuna mfumo rasmi wa uuzaji wa korosho lakini serikali ikaona itafute chombo imara ambacho kitasimamia wakulima na chombo kilichoonekana kinafaa ni chama cha ushirika. “Tukapewa dhamana ya kukusanya korosho ya wakulima pamoja na wanachama wetu kuiuza kwa mfumo wa stkabadhi ghalani sasa kwakua tumepewa jukumu na Bodi ya korosho imetoa mwongozo tukaona sisi kama wadau muhimu tuusome huo muongozo tuuelewe na tuape ili tuweze kutekeleza”Nalimi alisema”
Husna Mbata kiongozi wa chama cha ushirika Kilimahewa alisema”Tumeongea na wanachama wetu ambao pia ni wakulima na tumeongea nao kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani kama serikali ilivyoelekeza ili mkulima asiweze kunyonywa tena na tumewaambia wakulima wawe makini katika ukaushaji mzuri wa korosho”
Jumanne Makotwa Kiongozi wa chama cha ushirika kutoka Shungubweni alisema msimu uliopita baadhi ya wakulima walikuwa wakilazimisha kuleta korosho ambazo hazijakauka lakini kwa sasa tutawapa elimu ili walete korosho ambazo zitapata soko.
Makotwa aliongeza kwamba”tutahakikisha tunamwaga korosho zote chini ili kuhakikisha hakuna mchanga wala kokote kwenye magunia ya korosho”
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ina jumla vya vyama vya ushirika 48 ambavyo vinapatiwa mafunzo kwa lengo la kutekeleza majukumu yao pasipo kuvunja sheria katika uuzaji wa korosho kwa kutumia mfumo uliokubalika na Serikali ambao ni stakabadhi ghalani.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.